USAFIRI KUTOKA MOSHI KWENDA MIKOA MINGINE BALAA...MAMIA WAKWAMA JAPO WANA PESA




Mamia ya abiria katika kituo kuu cha mabasi Moshi wamejikuta wakishindwa kusafiri kama walivyotarajia kutokana na uhaba wa mabasi unaotajwa kuchangiwa na wingi wa watu wanaorejea mikoa mbalimbali baada ya kumalizika kwa Sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya.

Akizungumza leo Alhsmisi Januari 4, mwenyekiti wa wakala wa mabasi kituo cha Moshi, Wile Tuli amesema abiria wamekuwa wengi kwa kipindi hiki ikilinganishwa na miaka iliyopita.

Amesema adha ya usafiri imetokana na watu wengi kuanza kurejea katika shughuli zao baada ya kumalizika kwa sikukuu za mwisho wa mwaka, baadhi kupeleka watoto shule.

“Wapo waliokuja Moshi kwa magari binaasi, ila inavyoonekana magari hayo yalirudi na sasa wanapanda mabasi,” amesema,

“Jana abiria walikuwa wengi kuliko leo kutokana na kunyesha mvua kubwa hapa na usafiri kutoka vijijini umekuwa shida.”

Mmoja wa wakata tiketi ya mabasi ya kampuni ya Machame, Manase Ndosi amesema magari ni machache kutokana na abiria kuwa wengi.

Amesema Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) inapaswa kuongeza mabasi ili kuweza kunusuru abiria waliokwama kutokana na uhaba huo wa mabasi.

“Wengi nauli wanazo shida yao ni usafiri tu. Mfano leo kama mtu ana Sh40,000 eti ndio nauli yake, anataka tiketi aende Dar es Salaam. Kwa kuwa mabasi hamna amejikuta akishindwa kusafiri,” amesema.

Mmoja wa abiria, Dismas Mfoi amesema, “Hali ya usafiri hapa stendi ni ya shida, Sumatra ilitazame hili kwa kweli.”

Na Janeth Joseph,Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527