Monday, January 15, 2018

SERIKALI YAUFUNGUA MGODI WA BUHEMBA BUTIAMA

  Malunde       Monday, January 15, 2018
Hatimaye Serikali imefungua Migodi ya Dhahabu ya Wachimbaji Wadogo iliyopo katika eneo la Buhemba Wilaya ya Butiama Mkoani Mara baada ya kujiridhisha hali ya usalama katika migodi hiyo.


Migodi hiyo imefunguliwa rasmi na Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo Januari 13, 2018 na kushuhudiwa na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Annarose Nyamubi.


Akizungumza katika tukio hilo, Nyongo alisema jumla ya migodi 10 imefunguliwa kati ya 16 baada ya kujiridhisha usalama wake.


Alifafanua kwamba eneo la Buhemba lina jumla ya Migodi ya Dhahabu 16 ambayo inamilikiwa na Wachimbaji Wadogo hata hivyo iliyokidhi vigezo vya kiusalama ni Migodi 10 pekee ambayo imeruhusiwa kuendeleza shughuli za uchimbaji.


Alisema Serikali ilisitisha shughuli za uchimbaji Madini kwenye eneo hilo la Buhemba Februari 2017 baada ya kutokea vifo vya Wachimbaji Saba na wengine wapatao 15 kujeruhiwa kutokana na kufanya shughuli zao bila kuzingatia taratibu na kanuni za uchimbaji salama.


Alibainisha kuwa Mwezi Desemba mwaka jana alifanya ziara kwenye eneo hilo ili kujionea hali halisi ya machimbo husika pamoja na kuzungumza na wachimbaji waliosimamishwa kuendeleza shughuli zao ambapo aliagiza shughuli za ukaguzi zikamilike ifikapo Mwezi huu wa Januari ili migodi ifunguliwe.


"Kama mtakumbuka nilifanya ziara hapa na niliagiza kufikia Januari 10, 2018 Ukaguzi wa Usalama kwenye eneo la Machimbo ya Dhahabu ya Buhemba uwe umekamilika ili shughuli za uchimbaji zilizokuwa zimesimamishwa ziruhusiwe; tumejiridhisha mashimo kumi ni salama na sasa tunafungua rasmi," alisema Naibu Waziri Nyongo.


Alisema shughuli hiyo ya Ukaguzi kama alivyokua ameagiza ilifanyika kwa umakini na kwamba maduara Kumi (Migodi Kumi) yameruhusiwa na mengine Sita hayatoruhusiwa kuendeleza shughuli za uchimbaji.


Aliongeza kuwa baada ya kufika kwenye eneo hilo kwa mara ya kwanza alisikitishwa kuona wananchi wengi wakiwa wamekosa shughuli za kufanya kutokana na migodi hiyo kufungwa na ndiyo sababu ya kuagiza ukaguzi wake ukamilike haraka.


“Nilivyotembelea hapa Mwezi Desemba mwaka jana nilisikitishwa kuona shughuli za uchumi kwenye eneo hili la Buhemba zimesimama kutokana na shughuli za uchimbaji kusimamishwa baada ya kutokea ajali,” alisema.


Aidha, Naibu Waziri Nyongo aliwaagiza Wakaguzi wa Migodi kuhakikisha wanatembelea mara kwa mara maeneo ya migodi ili kukagua hali ya usalama pamoja na kutoa mafunzo ya uchimbaji salama kwa wachimbaji hususan wadogo lengo likiwa ni kuepusha ajali.


“Ninawaagiza kwa mara nyingine Wakaguzi wa Migodi kuhakikisha mnatembelea maeneo ya migodi mara kwa mara ili kuepusha ajali,” aliagiza Naibu Waziri.


Naibu Waziri Nyongo vilevile aliwaagiza wachimbaji madini kuhakikisha wanafuata sheria, kanuni na taratibu za uchimbaji ili kuepusha ajali migodini na wakati huohuo kunufaika ipasavyo na shughuli zao bila kupata usumbufu.


Aidha, Naibu Waziri alizungumzia ulipaji wa kodi na tozo mbalimbali ambapo aliwaagiza wachimbaji hao kuhakikisha wanalipa kwa mujibu wa sheria na alionya kwamba mgodi utakaoshindwa kulipa inavyostahili, utafungiwa.


"Tumewafungulieni migodi yenu tukiamini kwamba nanyi mtatimiza wajibu wenu wa kulipa kodi kwa mujibu wa sheria. Mkishindwa kulipa, hatutosita kuifungia," alibainisha Nyongo.


Naibu Waziri Nyongo yupo Mkoani Mara kwa ajili ya shughuli za ukaguzi wa migodi na kuzungumza na wachimbaji wadogo.
Usikubali kupitwa na habari..Pakua App ya Malunde1 blog HAPA Ili tuwe tunakutumia habari moja kwa moja Kwenye Simu yako
Loading...
logoblog

Kama Una Habari,Picha,Video,Tangazo n.k Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp +255 757 478 553 ,0625 918 527

Malunde 1 blog Ipo PlayStore....Pakua App yetu mpya HAPA Upate Habari Mpya Moja Kwa Moja Kwenye Simu yako..Utasoma habari hata kama hauna MB..Bofya Hapa
https://play.google.com/store/apps/details?id=com.malunde.blog
Previous
« Prev Post