DR WILBROAD SLAA AKUTANA NA RAIS MAGUFULI IKULU

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 29 Januari, 2018 amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi Mteule Mhe. Dkt. Wilbrod Peter Slaa, Ikulu Jijini Dar es Salaam.



Baada ya Mazungumzo hayo Balozi Mteule Mhe. Dkt. Slaa amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kumuamini na kumteua kuwa Balozi na ameahidi kuwa yupo tayari kutekeleza majukumu atakayopangiwa kwa kutanguliza maslahi ya Taifa.


Mhe. Dkt. Slaa amempongeza Mhe. Rais Magufuli na Serikali yake ya Awamu ya Tano kwa uongozi bora wenye maono na uthubutu wa kutekeleza mambo makubwa yenye maslahi kwa nchi ikiwemo miradi mikubwa kama vile ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge), ujenzi wa daraja la juu (Flyover) katika makutano ya barabara ya Nyerere na Mandela (Tazara), mradi wa uzalishaji umeme katika maporomoko ya mto Rufiji (Stieglers’ Gorge) na mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi.


“Kwa kweli naona faraja, ninafurahi Serikali ya Awamu ya Tano inatekeleza hatua kwa hatua karibu yote tuliyokuwa tunayapigania kwa miaka takribani 20 ya huko nyuma, na mimi Dkt. Slaa nilikuwa napiga kelele kwa sababu nilikuwa naona kuna upungufu.


“Leo ninasema ninafurahi yale niliyokuwa napigia kelele yanatekelezwa kwa sababu nimeyaona, sasa kitu kikubwa ni macho, ushabiki katika maendeleo hauna tija, ushabiki katika siasa nao hauna tija, kama nilivyowahi kueleza huko nyuma siasa ni sayansi, wapo wanaofikiri siasa ni upotoshaji na siasa ni udanganyifu lakini siasa ni sayansi, na siasa kama ni sayansi ina misingi yake inayohitaji kusimamiwa, na misingi yake ni nini kilikuwa ni tatizo na tatizo hilo linatatuliwa kwa misingi ipi, sasa haya tunayoyasema ni hivi, tulikuwa na tatizo la umeme, Stieglers’ Gorge inaanza kujengwa, na miradi mingine mikubwa inatekelezwa, haya ndio mambo ya msingi” amesema Mhe. Dkt. Slaa.


Kwa upande wake Mhe. Rais Magufuli amempongeza Mhe. Dkt. Slaa kwa moyo wake wa kizalendo na amesema aliamua kumteua kuwa Balozi kwa kuwa anatambua kuwa ataweza kupigania maslahi ya Tanzania popote atakapopangiwa kuiwakilisha.


“Dkt. Slaa alinijulisha kuwa anakuja na akaomba akija angependa kuja kuniona na nikampangia leo, tumezungumza mambo mengi na ameniahidi kuwa atakwenda kufanya kazi yake vizuri kwenye nchi atakayokwenda kuwa Balozi.


“Mhe. Dkt. Wilbrod Slaa ni mtu safi, anazungumza kutoka moyoni na anaipenda Tanzania na mimi kutokana na moyo wake wa kuchukia ufisadi na kuchukia wizi nikaamua kumteua kuwa Balozi” Amesema Mhe. Rais Magufuli.


Wakati huo huo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ameagana na maafisa wakuu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ambao wanastaafu baada ya kutimiza umri.


Walioagana na Mhe. Rais Magufuli ni Luteni Jenerali James Mwakibolwa aliyekuwa Mnadhimu Mkuu wa JWTZ na Meja Jenerali Michael Isamuhyo aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).


Wengine ni Brigedia Jenerali Aron Lukyaa, Brigedia Jenerali William Kivuyo, Brigedia Jenerali Elizaphani Marembo na Kanali Peter Samegi.


Akizungumza baada ya kuagana, Luteni Jenerali Mwakibolwa amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kumteua kuwa Mnadhimu Mkuu wa JWTZ na amesema anaondoka na kuliacha jeshi likiwa na nidhamu, utii, uzalendo na weledi.


Nae Meja Jenerali Isamuhyo pamoja na kumshukuru Mhe. Rais Magufuli amesema anafurahi kuiacha JKT ikiwa imeimarika katika majukumu yake yakiwemo ujenzi wa viwanda, kilimo na kuimarisha mafunzo kwa vijana wazalendo.


Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
29 Januari, 2018

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527