VIONGOZI WA DINI WATUMIA MKESHA WA KRISMASI KUICHANA SERIKALI KIAINA




 
Viongozi wa dini wametumia mkesha na ibada za Sikukuu ya Krismasi kuhimiza amani, upendo, kukemea maovu na kushauri viongozi wa Serikali kukubali kushauriwa na kutominya uhuru wa watu kutoa maoni.

Maaskofu, wachungaji na mapadri wa makanisa mbalimbali pia waligusia matukio ya utekaji na watu kutoweka.

Uhuru wa kutoa maoni, utekaji

Akizungumza katika Usharika wa Moshi Mjini, Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Mkuu wa kanisa hilo, Askofu Frederick Shoo alisema Watanzania hivi sasa wanajengewa hofu ili wasiseme ukweli wa kile wanachokiamini.

“Kuna watu wanajaribu kuwajaza watu hofu ili wasiseme ukweli na wasikae katika kweli. Watu wanajazwa hofu ili wasitetee kile wanachokiona ni cha haki,” alisema Dk Shoo.

Alisema, “Watu wanajazwa hofu ili wasiwe huru kutoa mawazo yao wanavyojisikia kuhusu Kristo, nchi yao na imani yao. Tukidumu katika kweli inatupa nguvu na uhuru wa kusema na kutembea bila woga.”

Askofu Shoo alisema, “Yesu amezaliwa si kutuletea tu neema, lakini anatuletea kweli kuhusu maisha ya hapa duniani. Mafundisho yanatufundisha tumpokee ili atawale maisha yetu.”

Alisema watu wanapaswa kudumu katika ukweli na daima wasimame katika ukweli na kutoona aibu wala woga wa kuusimamia ukweli huo.

Dk Shoo aliwataka waumini kutotumia sikukuu hiyo kufurahi na kujifurahisha wenyewe, bali kuwakumbuka watu wasio na furaha, amani, vyakula na mavazi.

Akizungumza katika Kanisa Katoliki la Kristu Mfalme, Jimbo la Moshi, Askofu Isaac Amani alisema matukio ya kutoweka kwa watu na mauaji ya kikatili kwa wasio na hatia yanayoshika kasi nchini ni ishara mbaya kwa Taifa.

Alisema Tanzania ya leo si ya miaka ya nyuma kwa kuwa watu wamekuwa na hofu kutokana na vitendo viovu.

Askofu Amani alisema kutoweka kwa watu na mauaji yanayoendelea nchini yanaleta hofu kwa wananchi, hivyo hatua za haraka zinapaswa kuchukuliwa ili kulinda amani.

“Matukio ya kutoweka kwa watu, mauaji ya wazee, albino, mashambulizi ya watu na imani za kishirikina ni maovu ambayo yanapaswa kuchukuliwa hatua ili amani idumu,” alisema Askofu Amani.

Aliwataka wananchi kuziombea familia zao na Taifa ili kudumisha upendo usio na unafiki na uwajibikaji akisema maombi hayo yatasaidia kuwapo kwa hofu ya Mungu na kuondoa tabia za watu wabinafsi wanaotaka kujilimbikizia mali bila kujali wengine.

Katika mahubiri yake, Askofu wa Kanisa Anglikana Zanzibar, Michael Hafidhi aliwataka viongozi wa Serikali kukubali kushauriwa na wenzao wa dini ili kuleta maendeleo.

Alisema kuzaliwa kwa Yesu kulileta mtafaruku kwa mtawala aliyeitwa Herode ambaye baada ya kushauriwa vibaya aliamuru watoto walio chini ya miaka miwili wauawe ikiwa ni mpango wa kumuua mtoto Yesu.

“Nampongeza Dk Ali Mohammed Shein (Rais wa Zanzibar) na Rais John Magufuli. Mungu awajalie hekima. Tunawaombea na tukiwapa ushauri wetu mzuri waupokee au ukiwa mbaya wauache,” alisema Askofu Hafidhi.

Akizungumza na mwandishi wetu baada ya ibada hiyo, Askofu Hafidhi alisema kumekuwa na urasimu kwa viongozi wa Serikali kusikiliza ushauri wa viongozi wa dini.


Alisema, “Tunawashauri kwa maendeleo ya jamii si mambo mengine. Kwa sababu usitegemee mimi nitakuwa Rais au waziri mkuu. Nafasi ya kuwashauri imekuwa ngumu mno kwa sababu ya urasimu wa watu wa chini. Viongozi hawana shida ila ule urasimu, inakuwa shida.”

Katika ibada iliyohudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Ayoub Ahmed Mahmoud na Mkuu wa Wilaya ya Mjini, Marina Thomas, askofu huyo pia alisisitiza kuhusu maadili ya familia.

Katika ibada nyingine iliyofanyika kwenye Kanisa Kuu la Roho Mtakatifu Dodoma, Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Central Tanganyika (DCT), Dk Dickson Chilongani alionya kuhusu viongozi kujifanya miungu watu badala ya kushuka kwa wananchi na kuwatumikia.

Alisema imekuwa ni tabia kwa wanasiasa wengi kufika kwa wananchi hasa kipindi cha uchaguzi lakini wanapochaguliwa husahau kuwatumikia.

“Krismasi hii iwe mfano bora wa kujishusha na kushuka kwa wananchi. Kuona shida zao na kuzitatua,” alisema.

Alisema, “Rais Magufuli anaweza kuwa mfano bora wa viongozi maana yeye ameshuka kwa wananchi na hasa wanyonge, ni fedheha kwa kiongozi aliyepewa dhamana na wananchi kujiinua na kujikweza badala ya kuwatumikia waliompa hiyo dhamana.”

Mchungaji wa Kanisa Anglikana la Mtakatifu Gabriel wilayani Kibaha mkoani Pwani, Emilius Haule alisema njia sahihi ya kuwabadilisha watu wanaojihusisha na vitendo viovu ni kuwapa elimu juu ya madhara yatokanayo na vitendo hivyo na si kuwachukia au kuwatenga katika jamii.


Amani na maadili ya viongozi

Akizungumza katika ibada iliyofanyika katika Kanisa Katoliki la St Peters jijini Dar es Salaam, Padri Paul Haule alisema amani ya kweli inapatikana kwa kumpokea Kristu na kuyaishi mapenzi yake sambamba na kutii sheria za nchi.

“Amani ya kweli ni zaidi ya kutokuwa na vita. Amani ya kweli ni pato la uadilifu na uadilifu ni kumpokea Mungu,” alisema Padri Haule.

Alisema ujio wa Yesu Kristu ni ishara ya amani na imeleta baraka na kutoa nafasi kwa binadamu kujipatanisha na Mwenyezi Mungu.

Alisisitiza waumini kuliombea Taifa ili lidumu katika amani ya kweli kuanzia kwenye familia.

Kuhusu kuliombea Taifa, Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Iringa, Tarriscius Ngalalekumtwa aliwataka wananchi sambamba na hilo, kudumisha amani.

Akizungumza katika Kanisa Kuu la Moyo Mtakatifu wa Yesu, Askofu Ngalalekumtwa ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), alisema amani ndiyo msingi wa ustawi wa Taifa.

Alisema watu kuishi maisha ya dhambi ndicho chanzo cha maovu kushamiri yakiwamo wizi, mauaji, ujambazi wa kutumia silaha na ubakaji.

Akihubiri katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Maurus, Kurasini jijini Dar es Salaam, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Polycarp Kardinali Pengo alisema ili kupata amani ya kweli duniani, wasitegemewe viongozi waliopo madarakani, bali wananchi wenyewe. Alisema kila mtu anapaswa kufahamu kuwa chimbuko la amani ni kufanya kazi halali inayopendeza machoni pa Mungu.

Aliwataka wananchi kuliombea Taifa na viongozi wake ili waendelee kusimamia ujenzi wa Taifa.

Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Dk Alex Malasusa aligusia mauaji ya raia akitoa mfano wa yaliyotikisa mkoani Pwani.

Katika Kanisa la Azania Front jijini Dar es Salaam, Dk Malasusa alisema, “Nashukuru mno kwa amani inayoendelea kuwepo katika nchi yetu hasa katika maeneo ambayo ilianza kufifia, ikiwemo Wilaya ya Kibiti.”

Katika hilo, Kardinali Pengo alisema mifumo ya kiutawala ya binadamu inapaswa kuzingatia maadili na kwamba, mikakati inayofanywa na viongozi inatakiwa kutosahau hilo akitaka hatua zichukuliwe ili kuwa na Taifa la kujitegemea.

“Tunaweza kufanya hivyo tukajikuta katika makosa yaliyoangusha mataifa mengi, tujaribu kuepuka hilo, ndiyo maana binafsi nafarijika kumsikia Rais na wasaidizi wake wanapoongelea kuhusu maadili,” alisema Kardinali Pengo na kuongeza:

“Tufanye kila linalowezekana kupiga hatua mbele lakini kamwe tusikubali hatua tunayopiga ikawa pembeni mwa Mwenyezi Mungu.”

“Tuombee jitihada za maendeleo kwa Taifa letu na tuwaombee viongozi wetu daima ili waweze kuweka mbele maadili katika kila hatua ya maendeleo nasi tukubali kuongozwa na maadili,” alisema.

Pia, aliwataka Watanzania kumuunga mkono Rais Magufuli katika juhudi zake za kufufua uchumi ikiwa ni pamoja na wananchi kufanya kazi kwa bidii.

Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Zanzibar, Augustino Shao alisema licha ya kuwapo kwa taarifa za uchumi wa nchi kukua, bado kuna hali ya umaskini kwa wananchi, huku baadhi ya viongozi wakizidi kuwa matajiri.

Akizungumza katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Joseph Zanzibar, alisema viongozi wasitumie nafasi zao kujilimbikizia mali wakati wananchi wengi wanazidi kuwa maskini.


“Wakati huu tunapotangaziwa kwamba uchumi wa nchi unapanda kwa asilimia saba, tunashuhudia umaskini mkubwa, hii ni alama kwamba uongozi wao ni mlango au fursa yakujilimbikizia mali,” alisema.

Alisema kiongozi makini ni yule anayewatetea wananchi anaowaongoza na lazima aakisi maisha yao.

Pia, aligusia amani na kubainisha, “Amani itatokana na kuwa na haki ya kweli, ndugu zangu viongozi kutakuwa na amani ya kweli kama kuna haki ya kweli kwa wengi, amani ya kweli ni katika haki.”

Paroko wa Kanisa Katoliki la Rumuli mjini Bukoba, Padri Faustine Kamuhabwa alisema kukumbukumbu ya kuzaliwa Yesu Kristo iendane na utamaduni wa kulinda maisha ya watu wengine.

Alisema pamoja na wajibu huo, binadamu wanawajibika kulinda na kutunza uhai wa mazingira.

“Kuna tishio la kupotea kwa amani katika nyakati hizi kwenye mataifa mengi duniani haki inapokiukwa eneo lolote huwezi kupata amani, kuna chuki na uhasama kuanzia ngazi ya familia ukiona hali hiyo kuna upande mmoja hautendi haki tuangalie mambo yanayoweza kutukosesha amani,” alisema Padri Kamuhabwa.

Askofu wa KKKT, Dayosisi ya Mashariki ya Ziwa Victoria, Andrew Gulle alisema, “Kuna kauli zimejengeka kuwa ukitaka kusema uongo, nenda kwenye siasa ndipo wanasema uongo, lakini jambo hilo si kweli hata kwenye siasa unatakiwa kusema ukweli na kutenda yaliyo mema kwa sababu Mungu ni mmoja na hapendi kuchukiza na kumfanyia matendo mabaya mwenzio.”

Suala la amani pia liligusiwa na Askofu wa Jimbo Katoliki la Shinyanga, Liberatus Sangu na Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Musoma, Michael Msonganzila.

Askofu Mkuu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima aligusia amani na kusisitiza kuwa hakuna mtu anayeweza kupata mafanikio kwa kuanzia juu na ikitokea hivyo basi ipo siku atashuka chini.

“Hata Yesu alizaliwa kwenye hori la ng’ombe, sehemu ya chini kabisa lakini ndiye aliyetukomboa na dhambi. Ogopa kilichozaliwa kwenye hori la ng’ombe, ukiona mtu ameanzia juu jua kuna siku atashuka,” alisema.

Katika mafundisho yake kwa waumini, Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam la Kanisa Katoliki, Eusebius Nzigilwa alisema kiburi na majivuno ni dhambi inayomtafuna mwanadamu.

“Sisi ambao tunapendelewa na kuonewa huruma na Mwenyezi Mungu, tumekuwa wakatili sisi kwa sisi, tunawekeana visasi na vinyongo,” alisema.

Mwenyekiti wa Kanisa la Moravian Jimbo la Ziwa Tanganyika, Charles Katale katika ibada mjini Kigoma alisema jukumu la kuilinda na kuitunza amani ni la kila Mtanzania.

Alisema duniani kumekuwa na tatizo la uhamiaji na ukimbizi ambalo limetokana na kutokuwa na amani.

“Watu wanaokimbia nchi zao na kwenda kuishi nchi nyingine si kama wamependa ni baada ya amani kutoweka, hivyo huhama kwenda sehemu salama ambayo amani inapatikana,” alisema Katale.

Chanzo- Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527