PESA ZA ASKOFU KAKOBE KUIZIDI SERIKALI ZAZUA BALAA....SASA TRA KUKOMAA NAE



Siku chache baada ya kiongozi wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship Askofu Zachary Kakobe kusema kuwa ana fedha nyingi kuliko Serikali, Mamlaka ya Mapato nchini TRA imejipanga kuanza kufuatilia ulipaji wake wa kodi.


Kamishna Mkuu wa TRA, Charles Kichere amesema mamlaka yake imeipokea kwa furaha kauli ya Askofu Kakobe na inataka kujiridhisha vyanzo vya utajiri huo.


Kichere amesema TRA inafahamu kuwa shughuli za kidini hazitozwi kodi lakini inataka kufahamu kama fedha hizo za Askofu Kakobe zinatokana na sadaka pekee au kuna shughuli nyingine za kiuchumi.


"Tumefuatilia hakuna kumbukumbu za Askofu Kakobe kulipa kodi, sasa tumeona tumfuate maofisa wetu wakajiridhishe kama fedha hizo anazozizungumzia zinatokana na sadaka,"


"Na kama hana shughuli zozote za kiuchumi ikiwa ina maana utajiri huo unatokana na sadaka ni jambo la kushtua kidogo lakini sisi tutaishia hapo,"


Amesema katika taarifa za mamlaka hiyo wapo watu wengi wenye fedha nyingi na kumbukumbu zao za kodi zipo lakini Askofu Kakobe si miongoni mwao.


Kichere amemwomba Askofu Kakobe kutoa ushirikiano kwa maofisa wa TRA watakaomtembelea kwa ajili ya shughuli hiyo ya ukaguzi.


Kuhusu kwanini uhakiki huo umekuja sasa Kichere amesema ni baada ya kusikia ana fedha nyingi kuliko Serikali wakati anafahamika ni kiongozi wa taasisi ya dini.

Na Elizabeth Edward, Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527