MAKAMBA : UONGOZI NI KOTI LA KUAZIMA



 Waziri wa Mazingira na Muungano, January Makamba ameamua kutumia sehemu ya siku za mwisho wa mwaka kuwakumbusha wenzake kuhusu nyadhifa wanazoshikilia.


“Uongozi ni koti la kuazima,” ameandika waziri huyo wa Ofisi ya Makamu wa Rais katika akaunti yake ya Twitter jana, Kama ilivyo kwa watumaji wengi wa ujumbe mfupi katika mtandao huo, Makamba hakutaka kufafanua kauli yake zaidi ya kuthibitisha kuwa iko kwenye akaunti yake.




Makamba, mmoja wa makada walio katika Baraza la Mawaziri la pili baada ya kuingia kwa mara ya kwanza wakati wa utawala wa Serikali ya Awamu ya Nne, ni mmoja wa watu wanaotuma ujumbe mara kwa mara katika mtandao huo.




Katika ujumbe wa jana, Makamba ameandika: “Uongozi ni koti la kuazima. Kuna wakati utarudisha tu. Kama ulikuwa unawakoga nalo watu, likirudi unaadhirika.”




Pamoja na kutoa tahadhari hiyo, Makamba bado hajakumbana na adha ya kupoteza uongozi tangu aondoke Ikulu ambako alikuwa mwandishi wa hotuba wakati wa Serikali ya Awamu ya Nne.




Baada ya kutoka Ikulu, mtoto huyo wa katibu mkuu wa zamani wa CCM, aligombea ubunge wa Bumbuli mkoani Tanga mwaka 2010 na kushinda na baadaye kuteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia kabla ya kushika wadhifa wa sasa.




Hata hivyo, Makamba ameshuhudia mawaziri wenzake kadhaa wakipoteza nyadhifa zao na kuwa wananchi wa kawaida, wakiwamo walioenguliwa kutokana na kashfa kama za Tokomeza, Escrow, makinikia, Tanzanite na wengine walioachwa katika mabadiliko ya kawaida ya Baraza la Mawaziri.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527