MWENDESHA BODABODA AMUUA KWA KISU MWENZAKE WAKIGOMBANIA ABIRIA


MWENDESHA bodaboda maarufu mpaka wa Sirari na Isebania, Kenya, Kiongera Nchagwa (27) mkazi wa Kijiji cha Gwitiryo, Tarime, Mara anasakwa na Polisi wa pande zote mbili, akituhumiwa kumuua mwenzake, Jeremia Omera (22) kwa kumchoma kwa kisu kifuani.

Mwenyekiti wa Haki za Binadamu Wilaya ya Kurya West ambaye pia ni Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wa Isebania, Peter Masaithe alieleza tukio hilo linatokana na ugomvi wa kunyang’anyana mizigo ya abiria aliyetaka kuvuka mpaka kuingia nchini akitokea Nairobi.

“Tukio hilo la mwendesha bodaboda Kiongera Mosaisi ambaye ni Mtanzania la kumchoma kisu kifuani mwenzake, Jeremia Omera Mgusuhi lilitokea Jumamosi asubuhi saa 1 katika stendi ya mabasi ya Nairobi, Isebania lililokuwa na abiria kutoka Tanzania,” alisema.

“Walianza kunyang’anyana mzigo wa abiria aliyeshuka basi la The Guardian akivuka kwenda Tanzania. Kila mmoja alidaka huo mzigo hivyo ugomvi ukatokea ambapo Kiongera alijihami kwa kisu na kumchoma kifuani Jeremia na akatokwa damu nyingi hali iliyopelekea kifo chake na Kiongera akatoroka kwa kutumia pikipiki yake na kuingia Tanzania,” alisema.

Masaithe alikemea bodaboda kutembea na visu, kunywa pombe za viroba ambavyo baada ya kupigwa marufuku sasa vimehamia Isebania hali inayochangia uhalifu na kuziomba serikali za nchi hizo mbili kuchukua hatua kali ukiwemo msako wa viroba na bangi ili kuokoa vijana.

Polisi wa Isebania wamethibitisha kifo cha Jeremia na wamewasiliana na wenzao wa Sirari kumsaka mtuhumiwa kujibu tuhuma. Polisi wa Sirari wamekiri kupokea taarifa ya mauaji.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Sokoni Sirari, Benson Makanya alisema waendesha bodaboda Sirari na Isebania wamekuwa wakitembea na silaha kama visu na kuchangia uhalifu hapo. Mama mlezi wa Jeremia, mkazi wa Sirari, Moraha Roman alisikitishwa na kifo chake na kusema alikulia kwao.

Aliiomba Serikali imfuatilie mtuhumiwa kwa madai mara nyingi akifanya matukio, hutorokea Mugumu, Serengeti kwa ndugu zake na kurejea baada ya muda. Mwili wake umehifadhiwa Hospitali ya Ombo Migori ukisubiri ndugu kutoka Soneka Kisii

IMEANDIKWA NA SAMSON CHACHA - HABARILEO TARIME

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post