MAPIPA 200 YA KEMIKALI YANASWA MWANZA

Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama imekamata mapipa 200 sawa na lita za ujazo 50,000 ya shehena ya kemikali bashirifu idhaniwayo kuwa ni ethyl alcohol.


Taarifa iliyotolewa na Kamishina wa Ukaguzi na Sayansi Jinai, DCEA, Bertha Mamuya jana Desemba 22 inaeleza kuwa kiasi hicho kilikamatwa Desemba 13 mwaka huu katika kivuko cha Kigongo wilayani Misungwi.


Alisema kemikali hiyo ilikuwa ikisafirishwa na kampuni ya Mwanza Lake Line Industiries kwenda mjini Kinshasa nchini DRC Congo, ikiwa kwenye gari linalomilikiwa na kampuni ya Mhili ya jijini Mwanza.


“Gari hili lilikamatwa likiwa halina nyaraka zinazoruhusu kisheria kusafirisha kemikali hizo,” alisema na kuongeza,


“Kitendo hicho ni ukiukwaji wa sheria namba tatu ya kemikali za viwanda na nyumbani ya mwaka 2003, na sheria ya dawa za kulevya namba tano ya mwaka 2015 na marekebisho yake ya mwaka 2017.”


Alisema kampuni hiyo ya Lake Line ikiwa inatambua kuwa imekiuka utaratibu za kujihusisha na kemikali, Desemba 14, iliidanganya mamlaka ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa kuomba kibali cha kutaka kusafirisha kemikali bashirifu na kupewa kibali hicho wakati tayari gari lenye kemikali hizo lilikuwa limeshakamatwa.


Alisema uchunguzi wa awali umeonyesha kuwa kampuni hiyo imewasilisha taarifa za uongo katika mamlaka mbalimbali za udhibiti, ikiwamo kiasi cha kemikali kilichokuwa kinasafirishwa na magari yaliyotakiwa kuisafirisha.


Alisema DCEA kwa kushirikiana na mamlaka nyingine inaendelea kufanya uchunguzi zaidi kuhusu kampuni hiyo na kwamba uchunguzi utakapokamilika, hatua zaidi za kisheria zitachukuliwa kwa wahusika.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527