KAULI YA MAGUFULI YAZUA GUMZO




 
Kauli ya Mwenyekiti wa CCM, Rais John Magufuli kuwataka viongozi wa Serikali kutii maelekezo ya viongozi wa chama hicho imeibua hisia tofauti kutoka kwa wasomi na wanasiasa.


Wakati baadhi wakiunga mkono kwa maelezo kuwa inalenga kuwakumbusha watumishi wa umma kutekeleza ilani ya chama hicho tawala, wengine walipinga wakisema haiendani na mfumo wa vyama vingi.


Rais alitoa kauli hiyo juzi alipokuwa akifunga Mkutano Mkuu wa CCM na kuwaonya viongozi wa Serikali akiwataka wasijaribu kukataa maelekezo kutoka kwa viongozi wa chama hicho kwani hata yeye anafuata wanachomueleza.


Alisema kiongozi wa Serikali katika ngazi yoyote anapaswa kutambua kuwa mwajiri wake mkuu ni CCM, “Mimi bila CCM nisingekuwa Rais. Chama ndicho kimejadili jina langu na tupo hapa kwa ajili ya kutekeleza ilani ya chama.”


Wakizungumza kwa nyakati tofauti Profesa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Benson Bana alisema kinachotekelezwa ni ilani ya chama kilichopo madarakani, hivyo wajibu wa kuisimamia na kuhakikisha inatekelezwa upo mikononi mwa chama chenyewe.


Profesa Bana alisema atamshangaa kiongozi wa umma wa kuteuliwa asiyetambua kwamba anafanya kazi chini ya chama hicho.


“Ilani ni mkataba baina ya chama, wananchi na waliochaguliwa hivyo ni lazima wanaofanya kazi chini ya Serikali inayoongozwa na chama husika wakubali kupewa maelekezo na kutekeleza maana kauli ya Rais inawakumbusha wajibu wao,” alisema Profesa Bana.


Lakini Profesa wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Ruaha (RUCU), Gaudence Mpangala alipingana na Profesa Bana akisema chombo kinachopaswa kuisimamia na kuidhibiti Serikali ni Bunge na si viongozi wa chama.


Alisema kutokana na mfumo wa vyama vingi, Serikali ikishaingia madarakani inao wajibu wa kuwatumikia wananchi wote bila ubaguzi.


“Kikatiba chama kikishaunda Serikali inakuwa ya Watanzania wote wakiwakilishwa na wabunge wao, kwa maana hiyo Bunge ndilo linalopaswa kuisimamia Serikali,” alisema Profesa Mpangala.


Mwingine aliyezungumzia suala hilo ni Dk Jimson Sanga wa Chuo Kikuu cha Iringa (UoI) ambaye alisema waangalizi wakuu wa utekelezaji wa kazi za chama ni viongozi wake.


Hata hivyo, alisema itakuwa vigumu kauli hiyo ya Rais kutekelezeka kwa sababu licha ya kuwa ilani inayotekelezwa ni ya CCM, mfumo uliopo ni wa vyama vingi.


“Kauli hii imeturudisha miaka ya nyuma ya chama na Serikali kuwa kitu kimoja yaani chama kushika hatamu, kwamba mtumishi wa umma ni sawa na mtumishi wa chama. Hii utekelezaji wake ni mgumu hasa kwa zama hizi,” alisema Dk Sanga.


Katibu wa CCM Mkoa wa Mwanza, Raymond Mwangwala alisema Rais Magufuli yupo sahihi kwamba ili kutekeleza ahadi za chama hicho kwa wananchi lazima viongozi wahakikishe wanaisimamia Serikali.


“Vipo vikao ambavyo lazima tusikilize ilani yetu ya chama imetekelezwaje. Kwa hiyo viongozi wa chama wanayo mamlaka ya kuhoji namna inavyotekelezwa kwa sababu tuliinadi kwa wananchi tutapaswa tena kuelezea utekelezaji wake,” alisema Mwangwala.


Alisema itakuwa rahisi kugundua maeneo ambayo shughuli za maendeleo zinasuasua kama viongozi wa chama wataweza kuisimamia Serikali waliyoiweka madarakani


“Hapa ni sawa na kumpa mtu akuuzie duka lazima upite kujua kama kuna faida au hasara ili uchukue hatua. Rais Magufuli yupo sahihi kabisa na ni lazima viongozi wa chama waache woga, waisimamie Serikali,” alisisitiza.


Hata hivyo, Mkurugenzi wa Itikadi na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema alisema agizo hilo linamaanisha chama kushika hatamu na si sahihi kwa wakati huu wa mfumo wa vyama vingi.


“Kama ndivyo, chama kinashika hatamu basi ni vizuri itangazwe pia kwamba, mfumo wa vyama vingi unafutwa vinginevyo, tutawashangaa watendaji wa umma wakitekeleza hili,” alisema.


Mrema alisema hofu ipo kwenye suala la wasimamizi wa uchaguzi ambao kama watapokea maelekezo ya chama na kufanyia kazi kipindi cha uchaguzi, haki haitatendeka kwa vyama vingine.


“Ukisikia chaguzi kuingiliwa hiyo ndiyo maana yake kwamba hata msajili akipewa maelekezo na kiongozi wa chama kwamba afute matokeo atafanya hivyo,” alisema.


Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen Kijo- Bisimba alisema kiutawala watumishi wa umma hawatakiwi kufungamana na chama chochote.


“Serikali lazima ihudumie vyama vyote, kuwa chama kinatawala haimaanishi kwamba kisikilizwe zaidi kuliko vingine, tupo kwenye mfumo wa vyama vingi hivyo Serikali haipaswi kufungamana,” alisema.

Na Tumaini Msowoya, Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527