MBUNGE MSIGWA ALAUMU UKIMYA WA WASOMI


Related imageIringa. Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa ametoa lawama kwa wasomi nchini akidai wamekuwa wakikaa kimya hata pale wanapoona masuala ya Taifa hayaendi sawa.

Mchungaji Msigwa amesema hayo wakati wa mjadala uliofanyika katika ukumbi wa Chuo Kikuu cha Katoliki Ruaha (RUCU) wakati wa kongamano kujadili kitabu kinachohusu miaka 70 ya kusaka demokrasia kwa nchi za ukanda wa Maziwa Makuu kilichoandikwa na Profesa Gaudence Mpangala wa chuo hicho.

“Kwanza nimpongeze Profesa Mpangala kwa kuja na utafiti huu ambao unaonyesha hali ya kidemokrasia nchini bado iko chini, nchi hii inawategemea ninyi wasomi ili iweze kusonga mbele, lakini kwa bahati mbaya mmetuachia sisi vipofu ndio tunaowachaguliwa njia ya kupita,” amesema Mchungaji Msigwa.

Amesema, “Upo usemi nimekuwa nikiutumia hata bungeni ‘akili ndogo kuongoza akili kubwa’ na leo hapa niwaeleze kuwa licha ya kuwa Taifa linawategemea, ninyi ndio mnaofanya tafiti bado mmeacha sisi wenye akili ndogo kuwachagulia ngoma ya kucheza nanyi mnakubali kuicheza hata pale mnapoona Taifa linatumbukia shimoni,” amesema.

Mchungaji Msigwa amewataka wasomi kutimiza wajibu wao na kuwataka kutumia elimu waliyonayo kushauri na kukosoa pale wanapoona inafaa kufanya hivyo.

Amesema hatua hiyo itasaidia Taifa kujenga misingi bora ya demokrasia inayoheshimu haki za binadamu na utawala bora na kusaidia kuinua uchumi wa nchi.

Mwandishi wa kitabu hicho, Profesa Mpangala amesema ili hali ya usawa wa kidemokrasia nchini iweze kufikiwa ni lazima kuandika Katiba mpya kwa kurejea maoni yaliyomo katika rasimu ya iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527