JENGO LA TANESCO KUBOMOLEWA KWA BOMU DISEMBA 11


JENGO la Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), sasa kubomolewa Desemba 11 mwaka huu huku Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), ikitafuta njia bora ya kubomoa jengo hilo ikiwemo matumizi ya bomu, baruti au kwa tingatinga.

TBA ambao wamepewa zabuni ya kubomoa jengo hilo, walishindwa kufanya hivyo Novemba 29 mwaka huu kutokana na mfumo wa kompyuta, uliotengenezwa kwa ajili ya utoaji wa huduma za umeme kwa njia ya luku, takwimu na samani mbalimbali zilizopo.

Akizungumzia ubomoaji huo Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mtendaji wa TBA, Eliud Mwakalinga alisema kuwa wanaendelea kutathmini njia bora ya kubomoa jengo hilo, kwa kuwa zote zina madhara kwa watu walio karibu na jengo hilo, ikiwemo uchafuzi wa hali ya hewa.

“Tunaweza kutumia teknolojia ya bomu kulipua jengo lote na kuisha, kutumia baruti kwa kuangalia nguzo nzito ili kubaki na kifusi au tingatinga. Lakini tumegundua kuwa bado kuna hali ya usalama tunatakiwa kuzingatia wakati wa ubomoaji ikiwemo vumbi litakalojitokeza, mawe na kokoto ambazo zinaweza kuharibu vioo vya wenye magari barabarani bila kujua,’’ alisema Mwakalinga.

Alisema kuwa wakati wa ubomoaji huo, watazungushia wavu sehemu ya jengo lote ili vumbi na kokoto zitakazotoka katika jengo hilo zisiweze kuleta madhara kwa watumiaji wengine wa barabara na wananchi wanaoishi karibu na jengo hilo.

Pia alisema jengo linapojengwa, hutumia michoro na kwamba hata kubomoa ni lazima watumie michoro ili kuona namna inayofaa katika kubomoa. Kwamba menejimenti yote ya TBA, ambao awali walitaka kuwapa watu wengine kazi hiyo ya ubomoaji, wamekubali kufanya hivyo kwa kuwa ni watumishi wenzao wa serikalini.

Novemba 27, mwaka huu uongozi wa Tanesco ulianza utekelezaji wa agizo la Rais John Magufuli, aliyeagiza majengo ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji na ghorofa la Tanesco, kuwekwa alama ya X kwa ajili ya kubomolewa.

Rais Magufuli Novemba 15, mwaka huu akitokea Chato alipokwenda kwa mapumziko baada ya ziara ya Uganda, aliagiza Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) kuweka alama ya X katika majengo hayo sehemu zilizo katika hifadhi ya barabara.

Tanesco ilisema baadhi ya watumishi wa shirika hilo, walianza kuhamishiwa katika ofisi nyingine za shirika zilizopo jijini Dar es Salaam ili kupisha shughuli za ubomoaji kufanyika kwa usalama.

Chanzo- Habarileo

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527