MHASIBU WA TAKUKURU MWENYE MALI NYINGI AYEYUKA.....ATAKAYEMUONA KUPEWA DONGE NONO

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imetangaza donge nono la Sh10 milioni kwa yoyote atakayefanikisha kukamatwa kwa aliyekuwa mfanyakazi wake Godfrey Gugai.


Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumanne Novemba 14, Naibu Mkurugenzi wa Takukuru, Brigedia Jenerali, John Mbungo amesema Gugai anatuhumiwa kujipatia mali nyingi kinyume cha Sheria ya Utumishi wa Umma.


Amesema kwa nafasi ya Gugai ya mhasibu wa taasisi hiyo ni vigumu kupata mali nyingi kiasi hicho.


"Awali tulipomhoji alitoa ushirikiano lakini tukiwa tunaendelea alitoweka na kwa taarifa tu amekuwa akitoka kwa magendo nje ya nchi, kwa yeyote atakayefanikisha kumpata tutamzawadia Sh10 milioni," amesema Mbungo


Amesema baada ya kutoweka walikwenda mahakamani kuhusu mali zake na tayari kuna zuio la kutokufanya kitu chochote yaani visiuzwe au kuendelezwa.

Baadhi ya mali anazomiliki mtuhumiwa ni pamoja na nyumba ya ghorofa nne iliyopo Ununio; nyumba ya ghorofa tatu iliyopo Bunju; nyumba za kupangisha zilizopo Mbweni JKT zote zikiwa jijini Dar es Salaam.

Nyumba nyingine iko Majita, Musoma; nyumba mbili zikiwa Kiseke na Nyegezi, Mwanza.

Zaidi ya nyumba hizo, anamiliki viwanja maeneo ya Bunju, Kigamboni, Mbuyuni-Temeke mkoani Dar es Salaam; Bagamoyo, Kibaha mkoani Pwani; huko Morogoro ana kiwanja huko Kihonda, Kiegea na Lukobe.

Viwanja vingine viko Kisasa, Itege na Kidachi mkoani Dodoma; vingine viko Nyegezi, Nyamanoro na Nyamagana mkoani Mwanza; ambapo ana viwanja vingine mikoa ya Musoma, Arusha, Tanga na kwengine.


"Kama atakuja na kutupa ushirikiano ikiwamo kuthibitisha uhalali wake basi tutamwachia mali yake lakini kwa nafasi yake kumiliki mali zote hizi zinatutia walakini," amesema


Naibu mkurugenzi huyo amewaonya watumishi wa umma kutokutumia vibaya madaraka yao waliyopewa kwani wakibainika hawatasita kuwachukulia hatua.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527