Simba na Yanga leo zimemenyana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mechi ya ‘kufa mtu’ ya Ngao ya Jamii kuashiria uzinduzi rasmi wa Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara msimu wa mwaka 2017/18.
Katika mchezo huo Simba imeshinda Ngao ya Jamii kwa kuifunga Yanga kwa mikwaju ya penati 5-4 baada ya timu zote kutofungana ndani ya dakika 90.
Hii ni Ngao ya Jamii ya tatu kwa Simba katika historia tangu kuanzishwa kwa ngao hiyo mwaka 2001.
Simba walitwaa kwa mara ya kwanza mwaka 2011 kwa kuifunga Yanga 2-0, mwaka 2012 wakabeba tena mbele ya Azam kwa ushindi wa magoli 3-2 kisha mwaka huu wameifunga Yanga kwa penati 5-4.
Yanga ndio timu pekee ambayo imechukua Ngao ya Jamii mara nyingi zaidi tangu ilipoanzishwa. Yanga imeshinda mara tano (2001, 2009, 2010, 2013 na 2014).
Azam na Mtibwa Sugar wamefanikiwa kuchukua Ngao ya Jamii mara moja moja.