SERIKALI KUNUNUA RADA NNE ZA KISASA TANZANIA

Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Anga (TCAA) jana (Jumanne) imeingia makubaliano na kampuni    inayojihusisha na mifumo ya anga kutoka nchini Ufaransa ya Thales kununua rada mpya nne.

Tukio hilo lilishuhudiwa na Waziri wa Ujenzi uchukuzi na mawasiliano Profesa Makame Mbarawa  na wadau wengine wa usafiri wa anga nchini. 

Upande wa Serikali mkataba ulisainiwa na Mkurugenzi wa Mkuu wa TCAA Hamza Johari na upande wa Thales alikuwa ni Meneja wa masoko wa kanda kutoka kampuni ya Thales Abel Aberr Carr.

Mkurugenzi wa Mkuu wa TCAA Hamza Johari anasema kwa sasa Tanzania ina rada moja pekee na uwezo wake kiufanisi umepungua kutokana na mabadiliko yanayotokea kwa haraka katika sekta hiyo, sanjari na kuongezeka kwa ndege zinazotumia anga la nchi.

“Mradi wa rada hizo ni miongoni mwa mipango mikakati iliyopewa kipaumbele cha juu na menejimenti ya TCAA kwa lengo la kuboresha huduma za uongozaji wa ndege kwa haraka, tija na kuongeza usalama katika sekta ya usafirishaji wa anga nchini na duniani,” amesema Johari.

Kwa upande wake Profesa Mbarawa amesema kufungwa kwa rada hizo kutaongeza imani ya wadau wa sekta ya usafiri wa anga dunia kuwa na imani na kutumia anga la Tanzania, hivyo watalii wataongezeka kwakuwa wanajua usafiri wa anga nchini kwetu ni wa usalama.

 “Kupatikana kwa rada hizo mpya tutaweza kutoa huduma kwa ndege nyingi zaidi na kulitawala anga letu zima. Ndege zikiongezeka na watalii wakaongezeka uchumi wetu utapiga hatua” alisema Profesa Mbarawa. 

Aidha kabla ya tukio hilo Waziri Mbarawa alitembelea chuo cha usafiri wa anga (CATC) ambapo alikutana na changamoto ya ufinyu wa eneo la chuo, ufinyu wa bajeti ya kununulia vifaa vya mafunzo na upungufu wa wataalamu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post