WAZIRI MKUU ATOA UFAFANUZI KUHUSU SERIKALI KUZUIA KUUZA CHAKULA NJE YA NCHI

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amejibu hoja zinazosambazwa na wanasiasa wa kambi ya upinzani juu ya zuio la chakula nje ya nchi, akisema Serikali haizuii fursa ya wakulima kuuza mazao nje.


Bali, amesisitiza serikali inataka mazao hayo yatosheleze nchini na kama ni lazima, basi kwanza yasindikwe, yabanguliwe, yachakatwe kwa kuyakoboa ili kuyaongezea thamani. Majaliwa alitoa kauli hiyo wakati akijibu hoja ya wapinzani, walioitisha mkutano wa waandishi wa habari juzi na kuilaumu serikali.


Alhamisi wiki iliyopita, wakati Waziri Mkuu akijibu swali la papo kwa hapo la Mbunge wa Viti Maalumu, Ritha Kabati aliyetaka kuruhusiwa kuuzwa mahindi nje ya nchi, alikataza kuuza mahindi nje ya nchi.


Alisema ni marufuku kuuza mahindi nje ya nchi; na kama ni muhimu lazima kibali kitoke kwa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa ajili ya kuuza nje ya nchi; na uuzwe unga uliosagwa na kamwe yasiuzwe mahindi.


Waziri Mkuu alitetea kauli hiyo ya serikali jana wakati akikagua banda la Ushirika wa Wakulima Wadogo wa Kilimo cha Umwagijiaji Dakawa (UWAWAKUDA) kabla ya kufunga Maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani (SUD), yaliyofanyika katika Ukumbi wa CCM wa Jakaya Kikwete mjini hapa.


Alimpongeza na kumsifu mkulima Nassib Katoto kwa niaba ya wakulima wenzake wa Mpunga Dakawa mkoani Morogoro, kutokana na kulima kilimo cha umwagiliaji, lakini hasa kuvuna mpunga, kuukoboa na kuusindika ili kupata mchele na kuuweka katika mifuko na kuuza baada ya kuongeza thamani, badala ya mpunga.


Majaliwa alisema nia ya serikali si kuzuia fursa ya wakulima kuuza mahindi nje ya nchi, bali inataka kuhakikisha kila eneo nchini linakuwa na chakula, kwani baadhi ya maeneo nchini hayana chakula kutokana na kukosa mvua na hivyo kukumbwa na ukame.


Lakini, kama ni lazima kuuza chakula nje ya nchi, basi ni vema kibali kikatolewa na Waziri mwenye dhamana kwa kuuza unga badala ya mahindi. 


Alisema mazao yakisindikwa, yakichakatwa, yakabanguliwa na yakikobolewa kama vile mahindi, viwanda vya kukoboa na kusaga vitapata kipato, watu watapata ajira na mabaki yake yaani pumba yatatumika kulisha mifugo, kuliko kama yangeuzwa mahindi, kwani viwanda visingepata kazi, vijana wasingepata ajira na mifugo isingepata chakula.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post