WATU WAWILI WAFARIKI BAADA YA KULA UGALI WA MUHOGO, SITA WALAZWA


WATU wawili wa familia moja wamefariki dunia katika kijiji na kata ya Kisumba tarafa ya Kasanga wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa na wengine 6 kulazwa katika zahanati ya kijiji hicho baada ya kula ugali wa muhogo.

Diwani wa kata hiyo Innocent Kukongwa alisema watu hao ambao ni wafamilia moja walikula ugali wa muhogo ambao
ulikuwa umeandaliwa kama chakula cha usiku ,ambapo baada ya
kula walianza kuharisha na kusababisha watoto wawili
kufariki dunia na wengine sita kukimbizwa zahanati kwa
matibabu zaidi.

Alisema baada ya kutumia chakula hicho waliamua kutumia dawa
ya kienyeji badala ya kwenda hospitali na kusababisha kifo kwa watoto hao.

"Inasikitisha kwani baada ya kula chakula hicho hawakutaka
kwenda zahanati na badala yake waliendelea kujitibu kwa kutumia
miti shamba na kushtuka baada ya kuona hali bado ilikuwa
ikiendelea kuwa mbaya",alisema Kukongwa.


Alisema baada ya tukio hilo kutokea waliamua kutoa taarifa
kwenye uongozi wa wilaya na kwa jeshi la polisi  ambapo
kwa pamoja walifika eneo la tukio.

Afisa tarafa ya Kasanga Peter Mankambila alisema watoto hao walifariki kwa kula chakula cha ugali wa muhogo.

Alisema kwa kawaida ugali wa muhogo huliwa maara baada ya kulowekwa kwa zaidi ya siku tatu inaonyesha familia hiyo ilikula ugali huo bila kuuloweka vizuri.

"Muhogo unaolimwa kwenye maeneo
haya ya Mwambao wa Ziwa Tanganyikahuwa ni mchungu kupita kiasi, hivyo bila kuuloweka
vizuri ni lazima ukuletee madhara kiafya kama ilivyotokea
kwa familia hii",alieleza.

Kamanda wa polisi mkoa wa Rukwa Geoge Simba Kyando alisema kuna taarifa mkanganyiko juu ya tukio hilo na kuahidi kutoa taarifa
zaidi mara baada ya uchunguzi.

"Kuna taarifa mkanganyiko kwenye tukio hili, kwani inadaiwa
kuwa familia hiyo ilitumia dawa ya kienyeji na zingine
zinadai kuwa walitumia ugali wa muhogo hivyo tunashindwa
kupata taarifa sahihi ni zipi, hivyo  nitatoa taarifa
zaidi uchunguzi ukikamilika na kubaini chanzo halisi cha vifo
vya watu hao’’,alisema kamanda Kyando.

Na Walter Mguluchuma- Malunde1 blog Kalambo

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post