TETEMEKO LA ARDHI LATOKEA KARAGWE KAGERA LEO JUMAPILI JULAI 30

Tetemeko lililodumu kwa takriban sekunde tano limetokea leo, Julai 30 saa nne asubuhi katika Mamlaka ya Mji Mdogo wa Kayanga wilayani Karagwe, lakini hakuna madhara yaliyoripotiwa kutokea.


Ofisa wa Wakala wa Jiolojia Tanzania, Gabriel Mbogani amesema ili kupata uhakika wa tetemeko hilo ni lazima kukusanya taarifa kwenye mitambo.


Amesema wananchi mkoani Kagera kwa sasa wapo makini baada ya kupatiwa semina kutokana na tetemeko la Septemba mwaka jana ambalo lilisababisha madhara makubwa.


“Wananchi wa Bukoba baada ya semina tulizotoa na kuwaonyesha ramani ya matukio ya tetemeko wamekuwa na uelewa, hivyo hata likitokea dogo kiasi gani lazima watoe taarifa,” alisema Mbogani.


Hata hivyo, amewataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari kwa kuwa haijulikani ni muda gani tetemeko kubwa linaweza kutokea kwa kuwa uzoefu ni kuwa huanza dogo na baadaye kuwa kubwa.


Mkazi wa mji mdogo wa Kayanga, Elieth Kikaka amesema alitoka nje ya nyumba baada ya tetemeko hilo kwa kuwa yamekuwa yakitokea mara kwa mara mkoani Kagera hivyo linapotokea ni lazima kuchukua tahadhari.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527