SERIKALI YAZINDUA JUKWAA LA USHIRIKA MKOA WA SHINYANGA


Mkuu wa wilaya ya Kishapu Nyabaganga Talaba akizindua jukwaa la vyama vya ushirika kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainabu Telack.


****

Serikali mkoa Shinyanga imezindua Jukwaa la Ushirika kwa lengo la kujadili maendeleo,changamoto pamoja na kuweka mikakati ili kuviendeleza vyama hivyo na kuviinua vile vilivyotaka kufa ikiwa vyama hivyo ndiyo silaha ya maendeleo kwa wanyonge na kuwainua kiuchumi.

Uzinduzi huo umefanyika leo Jumatano Julai 26,2017 katika ukumbi wa ofisi ya mkuu wa mkoa wa Shinyanga na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa maendeleo wakiwemo mameneja wa vyama hivyo vya ushirika na wawakilishi ,wakurugenzi wa halmashauri pamoja na mameneja wa taasisi za kifedha ili kupanga mipango ya kuviimarisha vyama hivyo ili viweze kufanya kazi kwa ufanisi na kuipeleka Tanzania kwenye uchumi wa kati.

Akizindua jukwaa hilo la vyama vya ushirika kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainabu Telack ,mkuu wa wilaya ya Kishapu Nyabaganga Talaba alisema ushirika ni muhimu sana kwenye nchi ambayo inataka kuendelea na kukua kiuchumi na hasa kwenye nchi ambayo inategemea uchumi wa viwanda.

Amesema vyama hivyo vya ushirika siyo vya kubeza kwani kwenye nchi ambazo zimeendelea kiuchumi vyama hivyo vimekuwa vikipewa kipaumbele na ndiyo maana rais John Pombe Magufuli ameamua kuvifufua kwa sababu anatambua umuhimu wa viwanda katika nchi ambayo inataka kukua kimaendeleo .

"Serikali ya viwanda bila vyama vya ushirika ni sawa na kazi bure ndiyo maana tumeamua kuzindua jukwaa hili ili kuunga mkono jitihada za rais wetu mpendwa kutaka Tanzania yenye viwanda" alieleza Talaba.

Talaba alisema serikali mkoani Shinyanga inataka kuiona SHIRECU mpya ambayo ni miongoni mwa vyama vikuu vya ushirika mkoani humo ikifuatiwa KACU vikifanya kazi kwa ubunifu na ufanisi ili kuwainua wakulima na pale wanapovuna mazao yao wapate pa kuyapeleka na kuyauza kwa bei nzuri ambayo itawainua kiuchumi.

Aliongeza kuwa kutokana na hali wakulima watahamasishwa kulima mazao mengi ambayo yataviwezesha viwanda kupata mali ghafi ya uzalishaji wa bidhaa na kukuza uchumi wa mkoa wa Shinyanga.

Aidha alisema viwanda vingi mkoani Shinyanga vimekuwa vikishindwa kufanya kazi vizuri na vingine kufungwa kutokana na ukosefu wa mali ghafi hususani vile ambavyo vinategemea malighafi ya mazao.

Katika hatua nyingine aliwataka wanachama wa vyama hivyo vya ushirika wanapoingia kwenye uchaguzi wa viongozi wao ,wachague viongozi walio na elimu ya vyama hivyo wenye weledi,uadilifu ambao watafanya kazi ya kuviendeleza vyama hivyo na siyo kuchagua viongozi wanaotanguliza pesa mbele.

Naye Kaimu Mrajisi wa vyama vya ushirika mkoani Shinyanga Dotto Maligisa alisema vyama hivyo mkoani Shinyanga vipo 412 kati ya vyama hivyo 168 , ni Sacco's,186 ni Amcos, 2 viwanda ,1 huduma,18 mifugo,3 nyumba 15 Madini na 9 ni vyama shughuli nyingine ,huku vyama vikuu viwili vikiwa ni SHIRECU ambayo inahusika na ununuzi wa zao la Pamba pamoja na Kacu zao la Tumbaku wilayani Kahama.

Akielezea kuhusu hali ya vyama hivyo vya ushirika wa mazao alisema (AMCOS) vina jumla ya wanachama 18,684 na wana jumla ya Hisa 9,028.8 zenye thamani ya Shilingi 90,288,00, Saccos zinajumla ya wanachama 18,642, hisa 54,592.27 zenye thamani ya Shilingi 545,922,740,Akiba za wanachama ni Shilingi 2,174,854,496.

Alisema kwa chama kikuu cha ushirika Shirecu ambacho kilianzishwa mwaka (1984) kina wanachama 700 wenye jumla ya hisa 1,073,936.17 zenye thamani ya Shilingi 5,336,980,860. 

Alitaja chama kingine kikubwa cha ushirika mkoani Shinyanga kuwa ni KACU ambacho kilianzishwa mwaka 1994 na kina wanachama 89 wenye jumla ya hisa 230 zenye thamani ya Shilingi 23,010,000.

Naye Kaimu Naibu mrajisi udhibiti na usimamizi tume ya maendeleo ya ushirika kutoka makao makuu alisema serikali ya awamu ya tano imeamua kuviinua vyama hivyo vya ushirika ,na wasipo vipiganie kurudisha heshima yake nchi hii haiwezi kuendelea wala kufukia uchumi wa kati na kutofanikisha falsafa ya Tanzania ya viwanda.

Alisema kutokana na dhamira ya serikali kuviinua vyama hivyo ,viongozi wabadhirifu hawana nafasi tena kwenye vyama hivyo ambao ndiyo waliosababisha kufa ,na kubainisha wale wote waliotafuna pesa watashughulikiwa ikiwa wameanza na chama cha ushirika Nyanza ambacho kipo jijini Mwanza kwa kuwashughulikia viongozi wote waliopiga dili kwa kuwafikisha mahakamani pamoja na kuwafilisi mali.

Aidha alisema vyama hivyo ni muhimu sana katika Tanzania ya viwanda ambavyo vitakuwa mkombozi kwa wakulima katika kupanga bei nzuri ya mazao ,kupatikana kwa uharaka pembejeo na kuepusha unyonyaji ambao amekuwa akifanyiwa mkulima na hatimaye kuendelea kuwa maskini na kusababisha kukata tamaa na viwanda kukosa mazao ya kuchakata bidhaa na hatimaye kuzoofisha uchumi wa viwanda.

Nao baadhi ya wanachama hao waliipongeza serikali kwa kuzindua jukwaa hilo la vyama vya ushirika na kuitaka pia izuie wanasiasa kutoviingilia kwenye utendaji kazi wao,ambapo wao ndiyo miongoni mwa vyanzo wa vyama hivyo kufa, pamoja na taasisi za kifedha kupunguza riba zao za mikopo ambazo zimekuwa kubwa na hivyo kukosa mitaji ya kujiendesha.

ANGALIA PICHA WAKATI WA UZINDUZI HUO
Mkuu wa wilaya ya Kishapu Nyabaganga Talaba akizindua jukwaa la vyama vya ushirika kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainabu Telack.
Kaimu Naibu Mrajisi Tume ya Maendeleo ya Ushirika Collins Benedict Nyakunga akizungmza kwenye jukwaa hilo na kuwataka wanachama hao wa Ushirika kuondoa mapungufu yaliyojitokeza hapo awali na kusababisha baadhi yao kudhoofika na vingine kufa kabisa ikiwamo kutokomeza masuala ya ubadhirifu wa fedha,utumiaji wa madaraka vibaya pamoja na usimamizi mbovu wa kuendesha vyama hivyo, lengo ni kurudisha heshima ya vyama hivyo vya ushirika.
Ofisa Ushirika Mkuu  Uhamasishaji na Uratibu Tume ya Maendeleo ya ushirika kutoka makao makuu Veneranda Adam Mgola, akizungumza ambapo alisema ili kurudisha heshima ya vyama hivyo vya ushirika ni vyema kufanya vikao mara mbili kwa mwaka kujadili maendeleo yao na changamoto ambazo hukutana nazo na kuzifatutia ufumbuzi sambamba na kusomea wanachama wao mapato na matumizi ili kuondoa mianya ya ubadhirifu wa fedha ambao ndiyo umeua vyama vingi vya ushirika hapa nchini, kutokana na kuendeshwa kiujanja ujanja.
Kaimu mrajisi wa vyama vya ushirika mkoani Shinyanga Dotto Maligisa akisoma taarifa ya vyama vya ushirika mkoani humo wakati wa uzinduzi wa jukwaa la vyama hivyo.
Mhadhiri kutoka chuo kikuu cha ushirika Moshi Gratian Cronery akizungumza kwenye jukwaa hilo kama miongoni mwa wadau wa vyama hivyo vya ushirika ,amebainisha tatizo lililosababisha vyama hivyo kuporomoka kiutendaji kazi kuwa uanzishwaji wake ulikuwa mwaka (1968) lakini (1976) vilifutwa na viliporudishwa mwaka (1984) vikarudi kama majeraha na hivyo kufanya kuendelea kuaguka mpaka leo sababu ya kukosa uelekeo.
Mhadhiri kutoka chuo kikuu cha ushirika Moshi Gratian Cronery alitaja sababu zingine kuwa ni ununuzi wa mazao kutozingatia bei elekezi, ujazwaji wa lumbesa,mizani mbovu,wanachama wa Ushirika kutokuwa wa kudumu,wanachama kutonunua hisa, kutokuwa na sera ya maendeleo ya ushirika,vyama vya ushirika kutegemea zao moja la kibiashara ambapo mavuno yake yakiwa hafifu navyo huzorota au kupotea kwa muda hadi pale mavuno yatakapopatikana tena ya zao hilo, na hivyo kuvitaka vijikite pia kwenye mazao mengine ya kibiashara ili kuendelea kilinda ubai wa vyama vyao na kuleta tija kwa wananchi na kukua kiuchumi kupitia sekta hiyo ya kilimo na viwanda.
Meneja wa chama kikuu cha ushirika mkoani Shinyanga (SHIRECU) Joseph Mihangwa akitoa neno kwenye jukwaa hilo ambapo alikiri chama hicho kushuka kiutendaji kazi na kuelekea kufa lakini bado kina uhai kwa kudai wana rasilimali (total asset) za Shilingi bilioni 4.47 na wanadaiwa na benki ya umma TIB kiasi cha Shilingi Bilioni 8.5 fedha ambazo walikopa mwaka (2013) kiasi cha bilioni 18 lakini mpaka sasa wameshalipa bilioni 14 pamoja na kulipa Riba bilioni 6 na kubakiwa na deni hilo la Bilioni 8.5 ambalo watajitahidi nalo walilipe .
Mihangwa alizitaja sababu za kuua vyama vya ushirika kuwa ni Kilimo cha Mkataba ambapo wanunuzi wa mazao kutoka viwandani walikuwa wanakwenda moja kwa moja kwa mkulima kulangua mazao yake bila ya kupitia vyama hivyo vya ushirika na hatimaye kusababisha kushindwa kujiendesha.
Makamu Mwenyekiti wa chama cha ushirika Bydemcos LTD kutoka Bulyanhulu Erasto Venus Mapato akichangia mada kwenye jukwaa hilo wakati wa majadiliano ambapo alibainisha changamoto nyingine iliyoua vyama hivyo kuwa ni wanasiasa ambao wamekuwa wakingilia utendaji wao kazi na kulazimisha kuungwa mkono kwenye masuala yake ya kisiasa na wakigoma hutafutiwa sababu za kuangushwa jambo ambalo ameiomba serikali wanasiasa wasiingie kwenye vyama hivyo vya ushirika ,huku akitaka sheria pia za vyama hivyo ziandikwe kwa lugha ya kiswahili ili wapate kuielewa pamoja na kuzitaka taasisi za kifedha kupunguza ukubwa wa riba za mikopo iliwapate fursa ya kukopa fedha na kuweza kujiendesha.
Wadau wa vyama vya ushirika mkoani Shinyanga wakifuatilia kikao cha uzinduzi wa jukwaa la vyama hivyo ,ambalo litasaidia kwenye mapinduzi ya ukuaji wa viwanda hapa nchini , hususani kwenye viwanda ambavyo hutumia malghafi ya mazao na kuifisha tanzania kwenye uchumi wa kati 2025.

Wadau wakiwa ukumbini

Wadau wa vyama vya ushirika mkoani Shinyanga wakifuatilia kikao cha uzinduzi wa jukwaa la vyama vya ushirika.

Picha na Marco Maduhu-Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post