MUASISI WA JINA TUMBILI KWA KAFULILA AIBUKA

Aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Fredrick Werema amezungumzia kauli yake ya mwaka 2014 ya kumuita ‘tumbili’ aliyekuwa mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila wakati wa mjadala wa Escrow bungeni, ambapo amesema ulikuwa msemo tu.


Jaji Werema ametoa ufafanuzi wa kauli yake ikiwa ni siku moja baada ya Rais John Magufuli kumsifu Kafulila kwa kuibua sakata la akaunti ya Tegeta Escrow na kumueleza kuwa yeye ni mtu safi na kwamba waliomuita tumbili ndio watakaokuwa tumbili.


“Unajua wengi walishindwa kuelewa nilisema nini, mimi nilichokizungumza ni kwamba tumbili haamui mambo ya msituni. Na huo ni msemo wa kawaida tu,” Jaji Werema anakaririwa na Mwananchi.


Hata hivyo, alikataa kuzungumzia kwa undani kuhusu kauli hiyo na sakata la Escrow akieleza kuwa watuhumiwa wa sakata hilo tayari wameshafikishwa mahakamani hivyo sio jambo jema kujadili suala hilo.


Mwaka 2014, kulitokea mvutano bungeni baada ya kafulila kuibua sakaka la Escrow ambapo Jaji Werema akiwa mwanasheria mkuu wa serikali alipinga vikali maelezo ya Kafulila akidai kuwa hajui anachokisema. Werema alimuita Kafulila ‘tumbili’, lakini mbunge huyo wa Kigoma Kusini alijibu kwa kumuita ‘mwizi’ huku akitaka uchunguzi ufanyike ili ifahamike ‘nani ni tumbili na nani ni mwizi’.


Kwa mujibu wa ripoti ya kamati maalum ya bunge, jumla ya shilingi bilioni 306 zilitolewa kinyamela katika akaunti maalum ya ‘Tegeta Escrow’ iliyokuwa imefunguliwa kwa pamoja na Tanesco na kampuni ya kufua umeme ya IPTL, ikisubiri usuluhishi wa Mahakama na ukokotoaji.


Hivi karibuni mmiliki wa kampuni ya VIP Engineering, James Rugemarila ambaye pia ni mmiliki mwenza wa kampuni ya IPTL pamoja na Mwenyekiti wa PAP, Habinder Seth Sigh wamefikishwa mahakamani wakikabiliwa na mashtaka ya uhujumu uchumi. Wawili hao wako rumande kutokana na mashtaka yao kutokuwa na dhamana.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post