MBOWE AMJIBU POLEPOLE KUHUSU KIGOGO WA CHADEMA ANAYETARAJIWA KUHAMIA CCM

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe amejibu kauli iliyotolewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole aliyesema kuna mtu mzito wa Chadema atakayehamia chama tawala hivi karibuni.

Mbowe amesema kuwa Chadema haiwezi kutetereka kwa kuondoka kiongozi yeyote kwani imejengwa katika misingi imara kama taasisi isiyotegemea mtu.

“Kwanza kabisa sitaki kuzungumzia propaganda za Polepole ambaye najua anajifunza siasa. Wapo wazito zaidi waliohama au kufukuzwa. Lakini niseme tu chama hiki kina misingi yake, mtu awe mdogo au mkubwa ni tafsiri tu, ingawa wapo wenye mchango mkubwa,” Mbowe anakaririwa na Mtanzania.

“Mtu yoyote anaweza kuondoka lakini Chadema kama taasisi itabaki imara. Mimi kama Mwenyekiti ninajua tumejenga taasisi imara ambayo haiwezi kutetereka kwa wanachama au kiongozi wa ngazi yeyote kuondoka,” aliongeza.

Kauli hiyo ya Mbowe imekuja wakati ambapo kumekuwa na matukio ya madiwani wa Chadema kuhamia CCM katika mikoa ambayo inasadikika kuwa ni ngome ya chama hicho kikuu cha upinzani kama Arusha na Kilimanjaro.

Mwenyekiti huyo wa Chadema ambaye pia ni Mbunge wa Hai amesema kuwa walifahamu hatua za madiwani hao zaidi ya 10 kufanya kile alichokiita usaliti hata kabla hawajatangaza kuhama.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527