LHRC YASIKITIKA WABUNGE WA CUF KUENGULIWA HUKU KUKIWA BADO KUNA KESI MAHAKAMANI


Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, (LHRC) kimetoa taarifa yake kwa vyombo vya habari kikisikitishwa na jinsi Bunge, lilivyotengua uteuzi wa wabunge wa viti Maalum juzi.

“LHRC inafuatilia mwenendo wa demokrasia nchini na kinatambua uwepo wa mzozo wa kiutawala ndani ya CUF, mzozo ambao umepelekea mgawanyiko ndani ya chama hicho na kufikia hatua ya wanachama kufikishana mahakamani kwa ajili ya usuluhishi,” imesema.

Taarifa hiyo iliyosainiwa na Kaimu Mkurugenzi wa LHRC, Anna Henga imesema LHRC ilitaraji kuona Bunge likiheshimu mhimili wa mahakama ambao bado haujatolea uamuzi shauri la Bodi ya Wadhamini ya CUF dhidi ya maamuzi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ya kumtambua Profesa Lipumba kama mwenyekiti.

“Kwa maamuzi haya bunge limedharau mhimili wa mahakama ambacho ni chombo huru kwa mujibu wa Katiba. LHRC kinalitaka Bunge kurejea maamuzi yake na kusitisha maamuzi hayo mpaka mahakama itakapochukua hatua.” Imesema taarifa hiyo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post