CHADEMA YATUMA SALAMU ZA RAMBIRAMBI VIFO VYA WATU 32 AJALI YA BASI ARUSHA

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kupitia Mkurugenzi wa Itikadi, Mawasiliano na Mambo ya Nje, John Mrema wametuma salamu za rambirambi kufuatia kutokea kwa ajali mbaya iliyotokea leo na kusababisha vifo vya watu 32.


Katika salamu zao cha CHADEMA wamesema wamepokea taarifa hizo kwa masikitiko makubwa kwani taifa limepoteza watu muhimu ambao wangelitumikia taifa katika siku zijazo.


"Tumepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za ajali mbaya Iliyotokea Leo tarehe 6 Mei,2017 Mkoani Arusha, Wilaya ya Karatu na kusababisha vifo vya wanafunzi 33 (watoto wa kike 16 na watoto wa kiume 17) waliokuwa wanafunzi wa Shule ya Lucky Vicent ya Mkoani Arusha.....Hakika taifa limepoteza watoto wake na vijana wa Kesho ambao wangelitumikia taifa letu siku zijazo". Alisema Mrema


Aidha, chama cha CHADEMA pia wametoa pole kwa familia ya wafiwa, uongozi wa shule ya Lucky Vicent pamoja na wananchi kwa ujumla.

"Kwa majonzi makubwa tunatoa salamu za pole kwa wazazi, wanafunzi wa Shule ya Lucky Vicent, uongozi wa Shule hiyo pamoja na wananchi wote wa Tanzania kwa msiba huu mkubwa na wenye kutia simanzi na huzuni kubwa...CHADEMA tutakuwa pamoja na familia za Marehemu katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo , tunawataka wanachama na watanzania wote bila kujali imani zetu tuwakumbuke wafiwa katika Sala /Dua ili Mwenyezi Mungu awatie ujasiri wafiwa katika kipindi hiki kigumu". Alisema Mrema


Pamoja na hayo, CHADEMA wamelitaka jeshi la polisi kufanya uchunguzi wa kina juu ya chanzo cha ajali hiyo mbaya ili matokeo ya uchunguzi huo yatumike katika kuzuia ajali nyingine isije kutokea katika siku zijazo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post