Angalia Picha : MAADHIMISHO SHEREHE ZA MEI MOSI 2017 UWANJA WA CCM KAMBARAGE SHINYANGA


Mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack akihutubia mamia ya wafanyakazi wa mkoa wa Shinyanga katika sherehe za Mei Mosi - 2017.

SERIKALI mkoani Shinyanga imetoa siku 14 kwa waajiri wote katika sekta binafsi mkoani humo kuhakikisha wanatekeleza kikamilifu Sheria ya Ajira na mahusiano kazini namba sita ya mwaka 2004 sambamba na kuwaruhusu wafanyakazi wao kujiunga na vyama huru vya wafanyakazi wanavyovitaka.

Agizo hilo limetolewa na mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack kwenye kilele cha maadhimisho ya sikukuu ya wafanyakazi duniani (Mei Mosi) zilizofanyika kimkoa katika kiwanja cha michezo cha Kambarage mjini Shinyanga baada ya kupokea maandamano makubwa ya wafanyakazi wa mkoa huo.

Hatua ya mkuu huyo kutoa agizo hilo inatokana na kilio kilichotolewa na katika risala ya Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) mkoani humo wakiiomba serikali iingilie kati tatizo la waajiri wengi katika sekta binafsi ambao kwa makusudi hawataki kutekeleza kikamilifu sheria ya ajira na mahusiano kazini.

Kutokana na hali hiyo mkuu huyo wa mkoa ametoa siku 14 kwa kila mwajiri aliyepo katika sekta binafsi kuhakikisha anatekeleza kikamilifu sheria hiyo kwa kuwapa wafanyakazi wao mikataba ya ajira inayotambulika kwa mujibu wa sheria ikiwemo kuwaruhusu kujiunga na vyama vya wafanyakazi wanavyovitaka.

Pia aliwataka waajiri hao kuhakikisha wanapeleka michango ya wafanyakazi wao katika mifuko ya jamii ili waweze kulipwa mafao baada ya kustaafu kazi na kwamba mwajiri anayeacha kupeleka michango hiyo anavunja sheria na anastahili kuchukuliwa hatua za kisheria.

“Nimeisikiliza risala yenu kwa umakini mkubwa sana na kuzisikia changamoto zote zinazowakabili, naahidi kuzipokea na zile zinazohitaji utatuzi wa ngazi ya kitaifa nitaziwasilisha kwa mamlaka husika ili zifanyiwe kazi mapema iwezekanavyo, na ambazo zipo katika uwezo wa ngazi ya mkoa, wilaya na serikali za mitaa, nitazifanyia kazi mwenyewe,”

“Hili la sekta binafsi kutotoa mikataba ya ajira, kuwazuia wafanyakazi kutojiunga na vyama vya wafanyakazi, kutotoa hati za malipo ya mishahara, kutolipa michango ya wafanyakazi kwenye mifuko ya kijamii, kutotoa likizo zote za kisheria, kutozingatia masaa tisa ya muda wa kazi kutokulipa saa za ziada na kutotoa vitendea kazi, yapo katika uwezo wa mkoa,” alieleza Telack.

Akikifanua alisema mwajiri ye yote anayewazuia wafanyakazi wake kujiunga na vyama vya wafanyakazi ni kinyume cha sheria ya ajira na mahusiano kazini namba sita ya mwaka 2004 kifungu cha 9 (1) (a) na (b) inayowapa haki watumishi kujiunga na vyama vya wafanyakazi.

“Sasa naagiza waajiri wote wa sekta binafsi kufuata sheria za kazi na kuondoa mapungufu hayo ndani ya wiki mbili kuanzia tarehe ya leo, ifikapo Mei 15, mwaka huu katibu tawala wa mkoa uunde timu maalumu itakayowahusisha makatibu tawala wa wilaya na wawakilishi wa vyama vya wafanyakazi na ofisi ya kazi mkoa,”

“Timu hii itafanya kazi ya kutembelea na kukagua katika sekta binafsi zote zilizopo katika mkoa wetu hususani hizo zilizotajwa hapa leo ndani ya risala ya wafanyakazi ili kuona kama zimetekeleza agizo langu, na endapo hawatatekeleza kwa vitendo nitachukua hatua kali za kisheria dhidi yao,” alieleza Telack.

Pia aliwataka wawaelimishe wafanyakazi waweze kutumia muda wao mwingi katika vituo vyao vya kazi kwa lengo la kuongeza ufanisi katika kuwatumikia wananchi sambamba na kufanya juhudi za kuongeza idadi ya wanachama ndani ya vyama vyao na wajenge mahusiano mazuri kati yao na waajiri.

Telack alisema kwa upande wake serikali ngazi ya taifa, mkoa na wilaya inaendelea na jitihada za kutafuta wawekezaji wakubwa na wadogo kutoka ndani na nje ya nchi katika sekta ya viwanda vitakavyotumia malighafi zinazotokana na kilimo na mifugo ili kuongeza wigo wa upatikanaji wa ajira kwa wananchi wa mkoa na Taifa kwa ujumla.

Awali katika risala yao kwa mgeni rasmi, Shirikisho la vyama vya wafanyakazi mkoani humo lilipongeza utendaji kazi wa serikali ya awamu ya tano iliyopo madarakani hivi sasa chini ya Rais Dkt. John Magufuli ikiwemo suala la kupiga vita vitendo vya rushwa, uzembe kazini, wafanyakazi hewa na waliofanya udanganyifu katika ajira kwa kughushi vyeti vya shule.

Pia waliupongeza uongozi wa serikali mkoani Shinyanga kwa hatua yake ya kusimamia suala la uboreshaji wa huduma za afya ambazo kwa sasa zinawafikia kwa uhakika wananchi walioko maeneo ya vijijini ambako pia wapo wafanyakazi wa kada mbalimbali za umma na sekta binafsi.

“Mheshimiwa mgeni rasmi, kwa heshima na taadhima tunaungana na watanzania wote kumpongeza kwa dhati Rais wetu wa serikali ya awamu ya tano, Dkt. John Magufuli kwa juhudi nyingi anazozifanya katika taifa letu kwa kupambana na mambo mbalimbali kama ufisadi, watumishi hewa, rushwa, madawa ya kulevya pamoja na vyeti feki,”

“Lakini pia tunaipongeza serikali kwa kuanzisha mfuko wa fidia kwa wafanyakazi (WCF) ambapo wafanyakazi wanapopata ajali wakiwa kazini wanalipwa fidia kupitia mfuko huo, sanjari na hilo tunaipongeza serikali mkoani Shinyanga kusogeza huduma za afya kwa wananchi wa vijijini,” ilieleza sehemu ya risala ya wafanyakazi.

Pamoja na pongezi hizo risala hiyo ilielezea changamoto mbalimbali zinazowakabili wafanyakazi mkoani Shinyanga hasa wale walioajiriwa katika sekta binafsi ambapo waliwataja kwa majina waajiri kadhaa wanaodaiwa kutotekeleza sheria ya Ajira na Mahusiano kazini namba sita ya mwaka 2004.

“Baadhi ya waajiri wa sekta binafsi hawatoi hati za malipo ya mshahara kwa wafanyakazi wao (salary slip), hawazingatii masaa tisa ya kazi na muda unapozidi hawalipwi posho ya muda wa ziada (overtime), hawalipi michango ya wafanyakazi kwenye mifuko ya jamii na huwanyima likizo zote za kisheria,”

“Hata hivyo serikali nayo kwa upande wake imekuwa ikikiuka mikataba ya mikopo ya elimu ya juu kwa kuwakata watumishi asilimia 15 kinyume cha mkataba ambao unaeleza wazi kiwango cha mtumishi kukatwa ni asilimia nane, hii ni sambamba na kodi ya mishahara kuendelea kuwa kubwa, tunaomba serikali itupunguzie makato haya,” ilieleza risala ya wafanyakazi.

Angalia picha matukio yaliyojiri katika uwanja wa CCM Kambarage wakati wa sherehe za Mei Mosi mwaka 2017-Picha zote kwa Hisani ya Mtetezi wa Haki Blog
Maandamano ya wafanyakazi kutoka sekta mbalimbali yakiendeleaWafanyakazi kutoka idara mbalimbali za serikali na sekta binafsi wakiwa katika maandamano ya Mei Mosi - 2017Wafanyakazi wa kampuni ya uchimbaji ya Acacia wakiandamana
Wafanyakazi wakipita kwa maandamano mbele ya mgeni rasmi katika sherehe za Mei Mosi - 2017.


Wawekezaji kutoka kampuni ya kichina ya Jielong pia walikuwa miongoni mwa watu walioshiriki sherehe Mei Mosi mkoani Shinyanga.Wafanyakazi, viongozi, waajiri na wananchi mbalimbali waliohudhuria sherehe za Mei Mosi - 2017 wakifuatilia matukio mbalimbali katika kiwanja cha michezo cha Kambarage.
Mratibu wa TUCTA Mkoa, Tabu Mambo (wa kwanza kulia) akiwa na Kaimu mwenyekiti wa TUCTA mkoa (wa pili kutoka kulia) mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack (mwenye kitambaa kichwani) mkuu wa wilaya ya Shinyanga, Josephine Matiro, mkuu wa wilaya ya Kahama, Fadhil Nkuru, mkuu wa wilaya ya Kishapu, Nyabaganga Talaba na Katibu Tawala wa mkoa, Albert Msovela wakipokea maandamano ya wafanyakazi katika kiwanja cha Kambarage mjini Shinyanga.
Mratibu wa sherehe za Mei Mosi - 2017, Filo Nchimbi kutoka chama cha Wafanyakazi wa mawasiliano na uchukuzi (COTWU "T") akisoma risala ya wafanyakazi mbele ya mgeni rasmi.
Kwa upande mwingine mkuu huyo mkoa amelitaka Shirikisho la vyama vya wafanyakazi (TUCTA) mkoani humo kuendelea kutoa ushirikiano chanya kwa serikali na wafanyakazi ili wafanye kazi kwa kujituma pasipo kuendelea kufanya kazi kwa mazoea.
Wafanyakazi pamoja na mgeni rasmi wakishiriki kuimba kwa pamoja wimbo maarufu wa wafanyakazi ufahamikao kama "Solidarity forever"

Pia palikuwepo na maonesho ya baadhi ya shughuli za wananchi.
Michezo ya kuvuta kamba na kufukuza kuku ilikuwa sehemu ya burudani zilizokonga nyoyo za wafanyakazi katika sherehe hizo.


Washereheshaji maarufu (MCs) Mwl. Msimbang'ombe Peter na Mwl. Tandise walikuwa makini katika kazi yao kuhakikisha mambo yote yanakwenda kama yalivyokuwa yamepangwa.
Picha zote kwa hisani ya Mtetezi wa Haki blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post