MAKONDA: SITISHWI,NAULIZA WEWE NI NANI UNINYAMAZISHE NA UMETOKA WAPI?

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, ameadhimisha mwaka mmoja wa kuwa kwenye kiti hicho kwa kula chakula cha mchana na waathirika wa dawa za kulevya, huku akizungumzia mafanikio aliyopata katika uongozi wake.

Licha ya kueleza mafanikio aliyopata, hakugusia kuhusu tuhuma mbalimbali zilizoelekezwa kwake na watu mbalimbali, badala yake alisema hakuna wa kumtisha wala kumnyamazisha na kwamba sasa ndiyo amepata nguvu mpya baada ya kupata mashambulizi mbalimbali.
Pia mkutano huo uliofanyika katika Ukumbi wa Maofisa wa Polisi, Oysterbay, Dar es Salaam, ulihudhuriwa na watu wachache wakiwamo waandishi kutoka vyombo vichache vya habari, tofauti na mikutano yake mingine ambayo alikuwa akialika vyombo vingi vya habari.
“Mwaka wangu wa pili katika uongozi ambao unaanza kesho (leo), speed (kasi) ya hali ya utumishi wangu itaongezeka mara mbili zaidi kwa sababu nimeshakomaa, lazima Dar es Salaam iwe kwenye mazingira salama.
“Eti mtu anataka nikae kimya wakati wananchi wangu wa Dar es Salaam wanateseka kwa matumizi ya dawa za kulevya… nauliza wewe ni nani uninyamazishe na umetoka wapi?” alihoji Makonda.
Alisema pamoja na changamoto nyingi anazopitia, hajawahi kutetereka wala kutingishwa na kwamba yuko tayari idadi ya wanaomchukia iongezeke kwa sababu hahitaji kupendwa.
“Sijawahi kutetereka wala sijawahi kutingishwa. Kazi hii nimepewa na Mungu, acha idadi ya wanaonichukia iongezeke kwa sababu sihitaji kupendwa, lakini niwe na uhakika na Mungu wangu.
“Mara nyingi ninapochapwa na mawimbi makali, mke wangu amekuwa akizama kwenye sala na kuniombea,” alisema.
Alisema anafanya kazi hiyo kwa upendo na kwamba hana kisasi na yeyote.
“Tunayafanya haya kwa upendo, hatuna kisasi na yeyote, ndiyo maana sisi tunafurahi, lakini upande wa pili wanapambana, kazi yetu ni kumulika watu,” alisema Makonda.
Aidha alisema wameamua kupigana vita ya dawa za kulevya hadharani kwa sababu hataki kupokea rushwa wala fedha haramu.
Makonda alisema kupitia fedha za dawa za kulevya, wengi wamejenga maghorofa na wamesababisha hata bei ya viwanja ipande, hivyo atahakikisha fedha hizo zinakauka ili kila mtu ale kwa jasho lake.
Alisema lengo lake ni kupambana kupigania ndoto za vijana na matumaini ya wazazi wao na haijalishi kama amechelewa, lakini hataacha.
Makonda alisema hababaishwi na watu wanaomchukia wakati akitekeleza majukumu aliyopewa na Rais Dk. John Magufuli kama Mkuu wa Mkoa.
Alisema wakiwaita wengine Kituo cha Polisi kwa vipimo, wamekuwa wakitumia dawa ya meno aina ya Colgate na chumvi, lakini sasa wamekuja na mbinu mpya ya vipimo.
“Wengine tukiwaita kwa ajili ya vipimo, kwa wale ambao wanapimwa kwa njia ya mdomo wanameza Colgate, wale wanaopimwa kwa njia ya mkojo wanaweka chumvi.
“Mnakumbuka wengine tulipowaita walikuwa wanachelewa kuja kumbe wanatumia vitu hivyo ili wasigundulike, sasa tuna mbinu mpya za kuwapima,” alisema Makonda.

MAFANIKIO YAKE
Akizungumzia mafanikio ya vita hiyo ya dawa za kulevya, Makonda alisema hadi sasa jumla ya waathirika 11,854 jijini Dar es Salaam wamekubali kuacha kwa hiari yao matumizi ya dawa hizo.
Alisema hivi sasa wamepewa eneo kubwa la kujenga kambi kwa wahanga wa dawa za kulevya, hivyo itawasaidia kufuatilia mienendo yao.
Makonda alisema amefanikiwa kumaliza biashara ya shisha, ambayo ilikuwa inatumiwa na baadhi ya wauzaji kuchochea matumizi ya dawa za kulevya.
Alisema pia, kwa kushirikiana na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishina Simon Sirro, wamefanikiwa kupunguza uhalifu wa aina mbalimbali, ikiwamo ujambazi wa kutumia silaha na vikundi vya uhalifu kama Panya Road.

MWAKA WA PILI
Makonda alisema kuanzia wiki ijayo moto utawaka katika maduka ya kubadilishia fedha (Bureau Change) kwa sababu zinatumika kuficha fedha haramu.
Alisema katika Mkoa wa Dar es Salaam, fedha chafu zilikuwa katika maeneo mawili ambayo ni bandari na dawa za kulevya, lakini sasa wamehamia katika Bureau de Change.
“Dar es Salaam hela chafu zilikuwa katika maeneo mawili; bandari na dawa za kulevya, lakini hivi sasa maeneo hayo dili limekauka wamehamia kwenye Bureau de Change… wiki ijayo moto utawaka, lazima tushughulike na maficho haya,” alisema Makonda.
Alisema hivi sasa wataanza mfumo wa kutumia kadi ili wakusanye kodi na kila mtu ale kwa jasho lake.
Makonda alisema katika mwaka wake wa pili ataanza ziara katika Serikali za Mtaa aone jinsi watendaji wanavyowasaidia wananchi.
Akizungumzia kuhusu wanaoishi mabondeni kama wana hati halali atawapatia viwanja, lakini watendaji waliotoa hati hizo atawashughulikia.
“Nawaomba wananchi wa Dar es Salaam wasikae maeneo hatarishi. Hatuwachukii bali tunawapenda sana, hayo si maisha mazuri… najua wengi wanaoishi mabondeni wamepangishwa na waliolipwa fidia, lakini huwezi kuwa na akili timamu ukakubali kupanga bondeni,” alisema.
Alisema pia utakuwa ni mwaka wa kuhakikisha utendaji wa watumishi wa umma unaboreka na wananchi waache kuzungushwa.
Alitolea mfano ofisi ya ardhi aliyosema imekuwa ikizungusha watu pale wanapotaka kupata vibali vya ujenzi.
“Ukitaka kibali watakusumbua, wakati mwingine watataka fedha ili waende kukagua eneo lako, kisingizo ni kwamba hawana bajeti, lakini ukijenga bila kibali watakuja kubomoa,” alisema Makonda.
Alisema kutoka na hali hiyo, asilimia 70 ya nyumba Dar es Salaam zimejengwa bila vibali.
Makonda alisema pia mwaka wa pili katika uongozi wake utakuwa wa kushukuru, hivyo kuwataka wananchi kujiwekea utaratibu wa kushukuru maofisa wa Serikali wanaotimiza vyema wajibu wao.
Mipango mingine aliyoieleza ni pamoja na kuelekeza maeneo ya kuuzia magari (showroom), kuhakikisha Mahakama ya Ardhi ya Kinondoni inatenda haki na kutoa hukumu kwa wakati na kwamba itafanya kazi hadi Jumamosi.

VITA DAWA ZA KULEVYA
Februari 2, mwaka huu, Makonda alitaja kwa mara ya kwanza majina ya baadhi ya wasanii, akiwamo Miss Tanzania 2006, Wema Sepetu na askari polisi aliodai wanahusika na dawa za kulevya.
Siku sita baadaye, alitaja majina mengine 65 ya watu maarufu akiwamo Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephati Gwajima pamoja na mfanyabiashara maarufu, Yusuf Manji akiwataka wafike Kituo Kikuu cha Polisi cha Dar es Salaam kuhojiwa juu ya tuhuma hizo.
Februari 14, mwaka huu, Makonda alikabidhi majina mengine 97 ya watuhumiwa wa dawa za kulevya kwa Kamishna wa Kupambana na Dawa za Kulevya, Rogers Siyanga ambaye aliahidi kutoyatangaza hadharani kabla ya kuyafanyia uchunguzi.

MAMBO AMBAYO HAJAYAGUSIA
Licha ya kuwapo kwa shinikizo kutoka kwa makundi mbalimbali ya watu, wakitaka Makonda ajibu tuhuma dhidi ya utata wa elimu yake na majina yake halisi, jana hakugusia kabisa mambo hayo, badala yake alionekana kuwajibu watu hao kwa mafumbo.
Hivi karibuni, watu mbalimbali akiwamo Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, wameibuka na kueleza utata wa jina la mkuu huyo wa mkoa pamoja na elimu yake.
Mara kadhaa, Askofu Gwajima amekuwa akisema jina halisi la Makonda ni Daud Albert Bashite na kwamba jina alilonalo sasa, alilipata baada ya kufeli mitihani yake na kuchukua cheti cha mtu mwingine alichokitumia katika masomo yake.
Mbali na hoja hizo, baadhi ya wabunge katika mkutano wa Bunge uliopita, walimtuhumu Makonda juu ya utajiri wake waliosema unatia shaka.
Baadhi ya mambo waliyosema ni umiliki wa magari ya kifahari na nyumba za kifahari zisizoendana na kipato chake.
Pia walisema moja ya kampuni binafsi imefanya matengenezo katika ofisi yake kwa mamilioni ya fedha.
Na ELIZABETH HOMBO-MTANZANIA DAR ES SALAAM

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post