MAHAKAMA YAGEUKA MBOGO KWA WANASHERIA WA SERIKALI KUMNYIMA DHAMANA MBUNGE GODBLESS LEMA


Mwenyekiti wa kikao cha jopo la Majaji watatu wa Mahakama ya Rufaa, kinachoendelea Arusha, Bernard Luanda, leo amegeuka mbogo kwa wanasheria wa serikali kwa kitendo cha kumnyima Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema dhamana kwa lengo la kumnyima haki.

Akizungumza Mahakamani hapo leo mbele ya majaji wenzake Stella Mugasha na Jaji Kipenka Mussa, Luanda amesema haipendezi na haingii akilini mtu (Lema) kushikiliwa kwa miezi minne bila sababu kwa misingi ya kumnyima haki.

“Tunaomba ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa serikai (DPP) muwe makini sana maana mnatufanya wanasheria wote hatuna akili na mnachafua Mahakama, kwa hali ya kawaida mtu mumshikilie kwa misingi ya kisheria, lakini katika kesi hii tumepitia jalada hatujaona kitu chochote cha kumshikilia Lema hadi leo na imetushitua sana,” alisema huku akishauriana na wenzake mara kwa mara kwa masikitiko.

Aliendelea kusema kuwa ofisi ya DPP inaitia najisi taaluma hiyo, kitu kipo wazi ila wanafanya vitu vya ajabu na havipendezi.

Alihoji jaji Luanda kuwa “Tumesoma faili lote tunashangaa hivi kweli ofisi ya mwanasheria mkuu ina wanasheria kweli na kama wapo kwa nini huyu mtu (Lema) awe ndani mpaka leo?”.

Alisema kwa kuwa mikono yao kisheria imefungwa hawawezi kufanya chochote kwa leo na kuwataka Mawakili upande wa Lema kurudi Mahakama Kuu, kuendelea na maamuzi ya dhamana.

Hali hiyo ilitokana na Wakili wa serikali Faraja Nchimbi kusimama mahakamani hapo na kuomba kuiondoa rufaa hiyo kwa madai kuwa ipo nje ya uwezo wake.

“Waheshimiwa Majaji baada ya timu yetu ya wanasheria kupitia kwa kina rufaa hii kwa sababu zisizozuilika tumeona hatupo tayari kuendelea na rufaa hii, maana hatukupeleka kusudio (Notisi) kwa msajili muda ulipita, hivyo tunaomba kuiondoa na uamuzi wa kuiondoa rufaa hii tumeufikia Ijumaa muda uliisha kuja mahakamani,”. Alisema Nchimbi.

Baada ya kuwasilisha ombi hilo, Wakili wa Lema Peter Kibatala, alisimama na kusema upande wao hawana pingamizi ila waliomba hoja za awali za rufaa hiyo ziondolewe Mahakamani hapo bila kunakiliwa.

Baada ya ombi hilo Jaji Kipenka Mussa alipokea kwa niaba ya Majaji wenzake na kukubali ombi la kuiondoa rufaa hiyo namba 9/2017.

Aidha Jaji Luanda alimkaribisha jaji Stella Mugasha pia kuongea kwa niaba yao ambapo alisema mahakama imekubali ombi la pili la kuiondoa rufaa namba 10/2017, baada ya Wakili Paul Kadushi kuomba kuiondoa pia.

Wakili wa Lema Peter Kibatala, alilazimika kusimama tena Mahakamani hapo kusema kuwa upande wao unasikitika kuona ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na DPP wanatumia Mahakama kwa njia ya kumnyima haki mteja wao, hivyo aliomba mahakama hiyo iwatatulie tatizo la kisheria lililojitokeza hadi mteja wao awe ndani hadi sasa.

Kibatala aliongea hayo huku akishindwa kujizuia na kumwaga chozi la huzuni mahakamani hapo mbele ya Majaji hao.

Via>>Mpekuzi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post