ASKOFU WA KKKT AONYA UCHU WA MADARAKA KANISA LA AICT DAYOSISI YA SHINYANGA

Askofu wa Kanisa la KKKT Dayosisi Kusini Mashariki ya Ziwa Victoria,Dkt. Emmanuel Joseph Makala
Askofu wa kanisa la AICT Dayosisi ya Shinyanga, Dr. John Nkola.
****

Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi Kusini Mashariki ya Ziwa Victoria,Dkt. Emmanuel Joseph Makala amewaonya waumini wa kanisa la Kanisa la African Inland Church Tanzania (AICT) Dayosisi ya Shinyanga kuepuka uchu wa madaraka baada ya askofu wa kanisa hilo Dkt. John Nkola kustaafu.

Askofu Dkt. Makala alitoa tahadhari hilo juzi katika ukumbi wa NSSF mjini Shinyanga wakati wa kikao cha kamati ya Maandalizi ya Mkutano Mkuu na sherehe za kumuaga Askofu wa Kanisa la AICT Dayosisi ya Shinyanga Dkt. John Nkola anayestaafu uaskofu mwezi Agosti mwaka 2017.

Askofu Dkt Makala wa Kanisa la KKKT Dayosisi Kusini Mashariki ya Ziwa Victoria alikuwa amealikwa kuwa mnenaji mkuu katika kikao hicho kilichohudhuriwa na wachungaji,wanakwaya na waumini wa kanisa la AICT kutoka ndani na nje ya mkoa wa Shinyanga.

Askofu Makala alisema historia ya makanisa mengi inaonesha migogoro inatokana na tamaa ya uchu wa madaraka miongoni mwa waumini hivyo aliwatahadharisha kumwogopa mungu na kuepuka kugombania madaraka kwani inaweza kusababisha mpasuko ndani ya kanisa.

Alisema asili ya binadamu yeyote ni tamaa ambapo aliwaonya waumini wa kanisa hilo kutomruhusu shetani kutawala nafsi zao wakati kumpata mrithi wa askofu John Nkola.

“Mungu awape rehema kwa sababu uchu wa madaraka ni wa binadamu na tumezaliwa na dhambi hiyo kwa sababu shetani aliyekuwa malaika alifukuzwa huko mbinguni kwa sababu hiyo hiyo”,alisema Askofu Makala.

“Askofu wenu anastaafu,hiyo roho ya uchu wa madaraka naomba muishinde kwa jina la yesu ili mnaporithisha uongozi mpya kwa taratibu zinazotakiwa basi askofu Nkola apumzike kwa amani na kanisa liendelee vizuri na kama patatokea vurugu kanisani mzee huyu mtamsononesha”,aliongeza Askofu Makala.

Hata hivyo aliwataka waumini wa kanisa hilo kuenzi mambo mazuri yaliyofanywa na askofu Nkola wakati wa uongozi wake na kuhakikisha kuwa wanafuata utaratibu unaotakiwa ili kumpata askofu mwingine.

Awali akizungumza katika kikao hicho Katibu Mkuu wa Kanisa la AICT Dayosisi ya Shinyanga,Mchungaji Jakobo Mapambano alisema askofu wa kanisa hilo Dkt.John Nkola aliyeanza kulitumikia kanisa hilo mwezi Oktoba 24 mwaka 1993 atastaafu mwezi Agosti mwaka huu.

Alisema kanisa hilo limeanza maandalizi ya sherehe ya kumuaga askofu Nkola na tayari kamati ya maandalizi inayoongozwa na Erasto Kwilasa inaendelea kufanya maandalizi na kwamba mgeni rasmi katika sherehe za kumuaga anatarajiwa kuwa rais John Pombe Magufuli.

Naye Mgeni rasmi katika kikao hicho,mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro alitumia fursa hiyo kuwaomba viongozi wa dini kuungana na serikali katika vita dhidi ya dawa za kulevya kwa kuweka ajenda ya dawa za kulevya katika mahubiri yao ili watu waache kuuza,kusafirisha na hata kutumia dawa hizo.

Aidha Matiro aliwaomba viongozi hao wa dini kutordhika na idadi ya waumini waliomo kanisani bali waendelee kuhamasisha watu wamjue mungu kwani watu wengi mkoani Shinyanga hawana dini.

Na Kadama Malunde-Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post