MBUNGE WA CHADEMA ALIYETAKA APIGIWE SALUTI NA POLISI ATUPWA JELA MIEZI 6 BILA FAINI


Picha ya maktaba ikimuonyesha mbunge Peter Lijualikali akiwa katika hekaheka na askari polisi. 

Mahakama ya wilaya ya Kilombero imemuhukumu kifungo cha miezi sita jela Mbunge Wa jimbo la Kilombero Peter Lijualikali (30) kwa kosa la kufanya fujo na kusababisha taharuki katika maeneo ya ukumbi Wa halmashauri ya Wilaya ya Kilombero

Mwendesha mashtaka inspekta Wa Polisi Dotto Ngimbwa aliiambia mahakama kuwa mshtakiwa, akiwa mshtakiwa namba moja pamoja na mwenzie Stephano Mgata (35) walitenda kosa hilo Machi mosi mwaka 2016 saa 4 asubuhi Kwenye kikao cha Baraza la Madiwani katika eneo la Kibaoni ukumbi wa halmashauri ya wilaya ya Kilombero.

Ngimbwa alisema washtakiwa hao kwa pamoja walifanya fujo kinyume na kifungu namba 89 kifungu kidogo cha kwanza B, cha kanuni ya adhabu sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2002, ambapo washtakiwa walikana mashtaka na hivyo kufanya kesi kusikiliza ushahidi wa pande zote mbili na upande wa mashtaka ukathibitisha shtaka bila kuacha shaka.

Hakimu mkazi katika mahakama ya wilaya ya Kilombero Timothy Lyon alisema mahakama imewatia hatiani kwa kosa hilo na kwa kuwa mshtakiwa Wa kwanza ni Mbunge ambaye alikuwa na kesi tatu huko nyuma na kutiwa hatiani amehukumuwa jela miezi sita.

Lyon alizitaja kesi za nyuma ambazo mbunge huyo alitiwa hatiani NA kuhukumiwa ni kesi namba 338 ya mwaka 2014, kesi namba 220 ya mwaka 2014 na kesi namba 340 ya mwaka 2014, hivyo kutokana na mshtakiwa ni mzoefu katika kesi zote, mahakama imemkuta na hatia ya kwenda jela miezi sita.

Hata hivyo mahakama hiyo imeona kwa kuwa mshtakiwa wa pili Stephano Mgata (35), hii ni Mara yake ya kwanza amehukumiwa kifungo cha miezi sita nje ambapo ndani ya kipindi hicho cha miezi sita hatotakiwa kutenda kosa lolote la jinai.

Hata hivyo katika hali isiyokuwa ya kawaida hali katika mahakama hiyo ilikuwa tulivu tofauti na kesi nyingine dhidi ya Mbunge Lijualikali, ambapo wafuasi wachache wanaodhaniwa kuwa ni wa Chadema ndiyo walijitokeza na baada ya hukumu kutolewa Mbunge huyo alipelekwa haraka gerezani kwenda kuanza kutumikia kifungo chake

Kutokana na jambo hili mwanasiasa Julius Mtatiro anasema kuwa licha ya Lijualikali kufungwa jela lakini hali hiyo haiwezi kupoteza ubunge wake na kusema kama akikata rufaa huenda akapata haki. 

"Hawezi kupoteza ubunge kwa kifungo hicho na kama akikata rufaa anaweza kupata haki, Kumfunga Lijuakali kwa sababu alihoji na kupinga kunyimwa haki yake ni kuzalisha Lijualikali wengi zaidi" alisema Julius Mtatiro 

Hivi karibuni mbunge huyo wa Kilombero, Peter Lijualikali kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) alimueleza Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba , kuwa hayupo tayari kutoa fedha za Mfuko wa Jimbo kuchangia kazi za maendeleo ya Polisi jimboni humo. 

Alisema hawezi kufanya hivyo, kwa sababu Polisi wa jimbo lake hawamtii na wanashindwa kumpigia saluti. 

“Hii ni hoja ya bungeni… mbunge kupigiwa saluti, lakini Polisi wa Ifakara hawanipigii saluti,” alisema Lijualikali, akimuarifu waziri huyo mwenye dhamana na jeshi la polisi. 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post