TAARIFA KWA UMMA KUHUSU DAWA ZA KUTIBU SUMU YA NYOKA TANZANIA

Kama tunavyofahamu, nchi yetu ina aina mbalimbali za nyoka ambao pindi wakimuuma mtu huleta madhara mbalimbali ya kiafya. Aidha tunafahamu kwamba tatizo hili lipo zaidi katika maeneo ya vijijini ambako uwezo wa wananchi kumudu gharama za matibabu ni mdogo.


Dawa za kutibu sumu ya nyoka huagizwa kutoka nje ya nchi. Dawa hizo siyo tu hazipatikani kwa urahisi, bali pia zinapatikana kwa gharama kubwa. Bei ya kununulia dawa hizi ni kati ya dola za kimarekani 55 hadi 85 (yaani shilingi za kiTanzania 118,250 hadi 182,750) kwa kichupa kidogo (vial) kimoja. Kichupa hicho huweza kutumika kwa wagonjwa wanne, lakini mara tu baada ya kufunguliwa dawa hiyo huwa haifai tena kutumika ndani ya mwezi mmoja tu.

Pamoja na changamoto hizo, Serikali kupitia MSD kila mwaka huagiza dawa hizi kwa ajili ya mahitaji hayo ya kutibu wagonjwa walioumwa na nyoka, ambapo bei ya kuinunua kutoka MSD ni TZS 200,000/= kwa kichupa kimoja. Hospitali zetu mbalimbali zimekuwa zikiagiza dawa hizi kutoka MSD na kwa washitiri wengine kwa bei hii au zaidi na kuwatibu waathirika wanaohitaji dawa za sumu za nyoka mara zinapohitajika. 

Napenda kuwakumbusha kwamba kwa mujibu wa Sera ya Afya ya mwaka 2007, huduma za tiba hutolewa bure kwa makundi maalum, au kwa kuchangiwa kwa sehemu ya gharama, au kwa kupitia mfumo wa Bima mbalimbali za Afya kama vile CHF. Kwa wale wasio na uwezo na wanaothibitishwa kuwa hawana uwezo, utaratibu wa msamaha hutumika.

Katika kuhakikisha kwamba wananchi wanaohitaji dawa ya sumu ya nyoka wanahudumiwa ipasavyo, Mhe. Ummy Mwalimu, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto anatoa maelekezo yafuatayo:-


Waganga Wakuu wa Mikoa na Viongozi wa Hospitali zote nchini wahakikishe kuwa Hospitali zote za umma zinaingiza dawa hii katika dawa za dharura ili iweze kununuliwa kama dawa zingine za dharura kupitia kifungu cha fedha za dawa za dharura. 

Kwa wagonjwa ambao watakuwa na Bima ya Afya, basi gharama za matibabu hayo zitalipwa kwa kupitia utaratibu huo wa Bima. Wananchi wanahimizwa kujiunga na Bima za Afya (CHF/NHIF) ili kupata unafuu wa matibabu haya na mengine. Mfano CHF - gharama ya kujiunga katika Halmashauri mbalimbali kwa kaya ni kati ya shilingi 5,000/= hadi shilingi 30,000/= kwa mwaka.

Kwa wagonjwa ambao watakuwa hawana Bima ya Afya, hao watatakiwa kuchangia gharama hiyo kwa nusu ya bei ya gharama ya dawa hizi au kwa kiwango kingine kitakachoamuliwa na Mganga Mkuu wa Serikali kadri itavyohitajika. 


Hii ni kutokana na ukweli kwamba kung'atwa na nyoka ni ajali na wananchi wengi wanaopatwa na ajali hii wapo maeneo ya vijijini ambao kimsingi uwezo wao wa kumudu gharama hizi kubwa za matibabu ya dawa ya sumu ya nyoka ni mdogo.

Wagonjwa watakaothibitika kuwa hawana fedha za kuchangia gharama hiyo, basi hospitali husika kwa kupitia mpango wa msamaha wa kulipia huduma za afya wahakikishe kwamba wanampatia mgonjwa huduma hizo kwa utaratibu wa msamaha wa gharama hizo.


Aidha, kwa kuwa nchi yetu ni kubwa na ina nyoka wengi, Mhe Waziri wa Afya anawaagiza Waganga Wakuu wa Mikoa na Halmashauri zote nchini kupitia kwa uangalifu takwimu za wagonjwa walioumwa na nyoka katika kipindi cha kuanzia mwaka 2013 hadi 2016 na kuziwasilisha Wizarani kabla ya tarehe 31 Januari 2017 ili kupata takwimu za mahitaji halisi ya dawa ya sumu ya nyoka nchini. Hii itasaidia kuboresha upangaji, uagizaji na upatikanaji wa dawa hizo nchini. 

Vile vile, Waziri wa Afya ameiagiza Bohari ya Dawa (MSD) kuweka utaratibu wa haraka wa kununua dawa hizo moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji ili kupata unafuu wa bei.


Imetolewa na:-
Nsachris Mwamwaja
Mkuu Kitengo cha Mawasiliano Serikalini - Afya
26/12/2016

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post