KAMPUNI YA NDEGE TANZANIA YATOA OFA MWEZI MMOJA SAFARI ZA DAR - MWANZA


Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) imetoa ofa ya mwezi mmoja kwa abiria wanaosafiri kutoka Dar es salaam kwenda Mwanza kulipa nauli ya shilingi 160,000/- kwa safari moja.


Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es salaam na na Kaimu Afisa Mawasiliano wa Kampuni Bi.Lily Fungamtama wakati akiongea na Idara ya Habari.


Amesema Ndege za Kampuni zimeanza kutoa huduma kuanzia Jumamosi ya wiki iliyopita ya tarehe 15 ya mwezi huu kama ilivyobainisha kupitia vyombo vya Habari.


Safari hizo zilianza kwa kutoa huduma ya kusafirisha abiria kuelekea nchini Comoro na hapa nchini itoa safari katika mikoa ya Mwanza, Arusha na Kigoma.


Bi.Fungamtama amesema kwa kuanzia walianza na mazoezi ya vitendo kwa marubani na wafanyakazi wa ndani ya Ndege ambapo hatimaye walianza safari za biashara ya kusafirisha abiria mnamo tarehe 15 Oktoba kama ilivyopangwa.


Ameongeza kuwa ATCL imeboresha huduma zake kwa kiasi kikubwa kwa kuwapatia wateja wake ofa ya kubeba kilo 20 za mizigo na kilo 7 za mzigo wa mkononi bure pamoja na kutoa vinywaji na ubadilishaji wa tiketi ni bure ndani ya mwezi.


Aidha, Kaimu Afisa Mawasiliano wa Kampuni Bi.Lily amekanusha taarifa potofu kuwa zimekwama kuanza safari zilizopangwa.


Amesema kuwa habari hizo sio za kweli kwani hivi sasa wameshaanza huduma katika mikoa hiyo mitatu.


Kampuni ya Ndege ya ATCL kwa sasa ina ndege tatu,zikiwemo mbili aina ya Dash8-Q400 zenye uwezo wa kubeba abiria 76 kila moja na Dash8-Q300 moja yenye uwezo wa kubeba abiria 50.
Na Daudi Manongi-MAELEZO

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post