ALIYETOBOLEWA MACHO NA SCORPION APEWA MAMILIONI YA FEDHA,AKUTANA NA DIAMOND PLATNUMZTangu mkazi mmoja wa Dar es Salaam Said Ally alivyoeleza namna alivyofanyiwa ukatili na kutobolewa macho yake mawili mbele ya umati wa watu katika eneo la Buguruni, watu wengi wamejitolea kwa hali na mali kumsaidia ili aweze kumudu gharama za maisha. 
Said Ally ambaye alieleza stori yake kupitia kipindi cha Leo Tena cha Clouds Fm, watu wameweza kumchangia fedha, vitu vyakumsaidia kuendesha maisha yake na vitakavyomuingizia kipato kwa sababu hawezi tena kufanya kazi kutokana na kupoteza uwezo wa kuona baada ya kutobolewa macho.Miongoni mwa misaada aliyoipokea hadi sasa ni pamoja na TZS milioni 10 ambazo amepewa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ambaye amesema kuwa yupo kwa ajili ya kuwasaidia wanyonge na wenye mahitaji kama alivyoagizwa na Rais Magufuli, lakini pia Makonda ameahidi kumlipia gharama aweze kufundishwa kusoma kwa kutumia alama na pia kumnunulia fimbo maalum ya kumsaidia kutembelea. Mbali na Mkuu wa Mkoa, Said amepewa msaada wa pikipiki 5 ambapo kati ya hizo, pikipiki 2 ni msaada Infotech na pikipiki 3 ni msaada kutoka TSN. Pia Adamjee amemsaidia Said Bajaji mbili ambapo vyote hivi vitaweza kumsaidia kuingiza kipato na kuendesha maisha yake. Vitu vyote hivi vimepatikana kutokana na jitihada zilizofanywa na Mkuu wa Mkoa wa Dar wa kutafuta watu wa kumsaidia Said. Kwa upande mwingine GSM kupitia ushawishi wa Mkuu wa Mkoa imesema kuwa itamsaidia Said Ally nyumba ya kuishi na yeye mwenyewe alishukuru sana na kusema kuwa angependa nyumba hiyo iwepo maeneo ya Tabata, Dar es Salaam kwani ndilo eneo alilolizoea kwani amekua akiishi hapo tangu mwaka 1999. Kwa upande mwingine, mwanamuziki Diamond Platnumz amejitolea msaada wa TZS milioni 2. Wakati Said akifanya mahojiano jana na Clouds Fm alisema kuwa moja ya vitu alivyo-miss kuvitazama ni pamoja na video ya Salome ya Diamond Platnumz, kitu kilichomsukuma mwanamuziki huyo kufika Clouds Fm na kutoa msaada. Said Ally ambaye ni baba wa familia ya watoto 5, kabla ya kukumbwa na mkasa huo wa kuharibiwa macho yake na mtuhumiwa Scorpion alikuwa akifanya kazi ya kinyozi Tabata.Mtuhumiwa aliyehusika na tukio hili tayari anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa uchunguzi kuweza kufanyika ili afikishwe mahakamani na haki iweze kupatikana.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post