Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SIMULIZI ZA MAJONZI WAHANGA WA TETEMEKO LA ARDHI KAGERA,WAFUNGUKA ILIVYOKUWA..INATISHA SANA



SEPTEMBA 10 haitasahaulika miongoni mwa wakazi wa mkoa wa Kagera.

Ilikuwa saa 9:27 jioni tetemeko la ardhi lilipokumba maeneo mbalimbali ya mkoa huu, huku mji wa Bukoba ukiwa mwathirika mkubwa. Hakuna aliyetegemea kama siku hiyo ingegeuka kuwa ya maafa kiasi cha kugharimu roho za watu 16 na mamia ya majeruhi. Kila mtu alikuwa kwenye shughuli zake kabla ya kuingia kwenye heka heka za kila mtu kujiokoa dhidi ya janga hilo.


“Kulikuwa na watu waliokuwa wamekaa eneo fulani katika maeneo ya Kashai wakiangalia mpira. Tetemeko lilipoanza, inadaiwa walidhani ni shambulio la kigaidi kwa hiyo waliposikia mtetemo, wote walilala kwanza…,” mmoja wa mashuhuda anasimulia. Mkazi wa kijiji cha Buhanga katika kata ya Buganguzi wilayani Muleba, Berna Nkalomba anasimulia kwamba, walikuwa kwenye tafrija kwa jirani yao. Wakiwa ndani, walisikia nyumba nzima inatikisika. Tulidhani kuna hitilafu ya umeme ndani ya nyumba. Tulianza kukimbia kwenda nje…ndipo tukagundua ni tetemeko la ardhi,” anasema Nkalomba.

Advera Respicius mkazi wa kijiji cha Rutenge, kata ya Kamachumu wilayani Muleba anabubujikwa machozi anapokumbuka namna janga hili la asili lilivyoandika historia ya majonzi kwake na familia kwa ujumla. Amempoteza binti yake, Verdiana, aliyekuwa na ujauzito wa miezi minane. Anasimulia namna alivyokumbwa na tetemeko akiwa kijijini kwake kabla ya dakika chache kupewa taarifa za kifo cha binti yake.

“Ilikuwa mida ya saa tisa alasiri … nilisikia kitu kama mlio wa katapila la kutengeneza barabara. Nikatoka nje lakini sikuona kitu na sikujua kama ni tetemeko,” anasimulia. Anaendelea kusimulia, baada ya dakika kama kumi nikiwa katika mshangao, nilipigiwa simu na mtu aliyeniuliza, unamjua Verdiana? Nikajibu ndiyo akakata simu.” Mama huyo anasema alipatwa na wasiwasi ndipo alipompigia Edo ambaye ni mume wa Verdiana aliyepokea simu akilia na kumwambia aende haraka Bukoba.

Alikimbia kwa ndugu yake na kupatiwa nauli ya kwenda mjini Bukoba. Akiwa ndani ya gari, anasema alisikia watu wanazungumza namna ambavyo tetemeko limeleta maafa makubwa ikiwamo vifo. “Nilipofika stendi, nilichukua pikipiki. Baada ya kufika nyumbani, nilichoshuhudia ni nyumba alimokuwa akiishi (Verdiana) imedondoka chini yote,” anasema Advera. Anasema swali la kwanza kwa mkwewe ilikuwa ni kuhusu aliko binti yake.

Anasema mkwewe alimwonesha kwa mkono kuashiria kuwa yumo ndani ya kifusi, taarifa zilizosababisha kupoteza fahamu. Alipozinduka, alikuta mwili wa binti yake umeshatolewa na kupelekwa hospitali ambako baada ya upasuaji, alitolewa mtoto wa kiume ambaye pia alikuwa amefariki. “Sikuwa na la kufanya. Tulirudi pale nyumbani kwa marehemu, na kulala chini ya mti ulioko jirani na nyumba mimi na wajukuu zangu watatu walioachwa na marehemu,” anasema mama huyu akilia na kuomba serikali kuwaangalia wote walioathirika na janga hilo.

Simulizi nyingine ya huzuni inatoka kwa Alex Felex, mkazi wa kata ya Hamgembe aliyepoteza mtoto na mke katika janga hilo.

Anamtaja mkewe Lucy na mtoto wao Alisia akisema, “tulikuwa dukani mimi na mke wangu na mtoto wetu. Ilipofika saa nane na nusu akaamua kwenda nyumbani ambako ni karibu na dukani kwetu ili akachukue chakula na mara nyingi huwa akienda anatumia nusu saa kurudi lakini kabla ya nusu saa likatokea tetemeko.”

Anasema alipokwenda nyumbani, alikuta ukuta mmoja wa nyumba umeangukia ndani na mwingine nje. “Nikaingia ndani haraka haraka nikaanza kumuita mke wangu hakuitika, nikatazama huku na huku sikumuona mke wangu wala mtoto wangu ,nikaamua kufukua kifusi cha ukuta wakati nikiendelea nikaona kipande cha khanga ya mke wangu,”anaeleza huku akibubujikwa na machozi.

Majeruhi Stanislau Frances aliyelazwa katika Hospitali ya mkoa wa Kagera, anasimulia kuwa alikuwa miongoni mwa watu waliokuwa kwenye tafrija ya kipaimara kabla ya tetemeko kuwakumba. Frances anasema alikuwa amewatembelea ndugu zake hao waliokuwa na tafrija.

“Wakati sherehe zikiendelea, tulisikia mtetemo tukadhani ni hitilafu ya umeme,” anasema. Anasema walianza kukimbia kuelekea nje lakini yeye kabla ya kutoka, aliangukiwa ukuta kwenye kiuno na miguu, akazimia na kisha kujikuta yuko hospitalini. Kijana huyu anatamani wangekuwa na elimu mapema juu ya majanga kama haya na namna ya kujiokoa. Anasema ingekuwapo, wapo watu ambao wasingepoteza maisha au kujeruhiwa.

Changamoto hii ya jamii kutokuwa na elimu ya kutosha juu ya tetemeko, inajidhihirisha pia kutokana na simulizi kwamba, kuna watu waliokuwa wakiangalia mpira wa miguu kwenye televisheni katika eneo la Kashai, mjini Bukoba. Baada ya kusikia mtetemo, inadaiwa walichofikiria ni matukio ya ugaidi. Inadaiwa wote walilala chini wakiamini lipo shambulio. Lakini baadaye ndipo walibaini ni tetemeko la ardhi.

Mkazi wa Maruku, Bukoba Vijijini, Anastazia Laulian (79) anakiri kwamba katika umri huo, hajawahi kushuhudia tetemeko kubwa kama hilo. Bibi huyu ambaye ni majeruhi aliyelazwa katika Hospitali ya mkoa wa Kagera kwa kuumia mguu baada ya kuangukiwa na mlango pamoja na matofali, anasema tetemeko analokumbuka ni la mwaka 1968 wakati akinyonyesha mtoto wake wa tatu aitwaye Auleria.

“Nilikuwa mdogo. Unajua wakati huo zamani tulikuwa tukiolewa tukiwa na umri mdogo, nilikuwa ndani siku hiyo namnyonyesha mtoto wangu nikasikia mtetemo kwenye nyumba nikahisi kama vile kuna jini kaingia ndani ya nyumba nikakimbilia uvunguni mwa kitanda na mtoto wangu, lakini ilichukua muda mfupi kama dakika tatu tu ila halikuwa kubwa kama hili wala nyumba hazikubomoka baadaye ndio niliambiwa na mama mkwe kuwa ni tetemeko,”anaeleza Anastazia.

Hata hivyo anasema aliwahi kusimuliwa na baba yake kuwa pia mwaka 1947 lilitokea tetemeko lakini akisisitiza kuwa halikuwa kubwa. Bibi huyu anaongeza tetemeko hili la ardhi kwenye orodha ya majanga makubwa yaliyowahi kutikisa mkoa wa Kagera na kuandika historia ya huzuni. Anataja majanga hayo ni pamoja na vita ya Kagera, utekaji wa kutumia silaha uliokuwa ukifanyika katika mapori mbalimbali, baa la njaa ‘ibambula mabati’ iliyotokea mwaka 1945 na ugonjwa wa Ukimwi .

“Matukio kama hayo yalikula maisha ya watu wetu na kutuingiza katika umasikini. Sasa leo nyumba zetu zimeanguka, hatuna pa kulala tunahangaika wengine hatuna watoto wa kutusaidia,” anasema bibi huyo. Anaendelea kushuhudia ukubwa wa janga hili akisema, walizoea kuyasikia katika nchi za mbali. Mkazi mwingine wa Bukoba Mjini, Savelina Mwijage anasema, “janga hili limenigusa sana. Nimelifananisha na janga la meli ya Mv Bukoba lililochukua maisha ya wenzetu,s ina la kusema tumeumia sana.”

Kwa ujumla, walioathirika na tetemeko hili la ardhi ni wengi na wenye simulizi zenye kusababisha kutokwa machozi. Kwa mujibu wa Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Deodatus Kinawilo imeundwa kamati ya kufuatilia athari .

Taarifa za awali zinaonesha, inakadiriwa wananchi waliokosa makazi ni zaidi ya 3,000. Athari haziko Bukoba Mjini pekee bali Mkuu wa Mkoa, Salum Kijuu anataja wilaya za Bukoba, Missenyi, Muleba na Karagwe zimekumbwa pia. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliyetembelea wananchi walioathirika, anawasihi kuwa wavumilivu na kushirikiana na serikali katika kutatua changamoto wanazokumbana nazo ndani ya kipindi hiki cha majonzi.
Imeandikwa na Angela Sebastian-Habarileo

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com