CHADEMA Yaandaa Vijana 4,000 Kwa Ajili ya Kuzuia Mkutano wa CCM Dodoma

BARAZA la Vijana la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (BAVICHA) limeendeleza msimamo wake wa kuzuia Mkutano Mkuu Maalum wa CCM, uliopangwa kufanyika Julai 23, mwaka huu mjini Dodoma.


Katika kuhakikisha linatimiza azma yake hiyo, baraza hilo limesema wanachama wake wapatao 4,000 wamejiandaa kushiriki kwenye shughuli hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, baada ya kuhojiwa kwenye Kituo Kikuu cha Polisi, Makamu Mwenyekiti wa Bavicha, Patrick ole Sosopi, alisema kuna vijana watakaotoka sehemu mbalimbali ili kuzuia mkutano wa CCM.

Sosopi alisema Bavicha watakwenda Dodoma kuzuia Mkutano Mkuu Maalum wa CCM kwa kile walichodai kusaidia Jeshi la Polisi kutekeleza amri yake ya kuzuia mikutano ya kisiasa hadi 2020.

Alisema pia kuna watu wamejitolea kutoa magari kwa ajili ya kuwabeba vijana hao ili kuwafikisha Dodoma kuunga mkono agizo la polisi.

Sosopi pia aliomba Jeshi la Polisi kuwachukulia hatua viongozi wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) kutokana na kauli zao za vitisho walizozitoa dhidi ya Bavicha hivi karibuni.

Akizungumza na waandishi wa habari Julai 4, mwaka huu, Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka Hamad Shaka, aliionya Bavicha wasiende Dodoma kuzuia Mkutano Mkuu Maalum wa CCM kwa kuwa watatumia kila mbinu kuwazuia ili kulinda heshima ya chama chao.

Sosopi alisema wao hawataki matatizo wala vurugu bali wanachofanya ni kutii agizo la polisi kwa unyenyekevu.

"Mkuki kwa nguruwe kwa binadamu mchungu kwani Rais alipopiga marufuku mikutano ya kisiasa hadi 2020, CCM walichekelea wakiamini kuwa Chadema tumekomolewa lakini iweje sasa Jeshi la Polisi likubali kuruhusu mkutano wao wakati Chadema hata mikutano ya ndani tunazuiliwa?

"Hatutanii hata kidogo na wala CCM wasidhani kuwa hatutakwenda Dodoma lakini tunaliomba Jeshi la Polisi litende haki juu ya kauli za uchochezi kwani nilitegemea viongozi wa UVCCM wangekamatwa na jeshi hilo lakini tunaokamatwa ni sisi tu," alisema Ole Sosopi.

Akizungumzia suala la kuhojiwa na polisi jana, Ole Sosopi alisema alikuwa kituoni hapo kuhojiwa kwa kosa analodaiwa kufanya Juni 18, mwaka huu la kutoa kauli za uchochezi.

Sosopi alikamatwa mara ya kwanza Juni 26, mwaka huu mkoani Iringa na kusafirishwa hadi jijini Dar es Salaam na
kuhojiwa kwa kosa hilo katika shughuli ya mahafali ya wanachama wa Chadema waliomaliza vyuo vikuu.

Sosopi alisema baada ya kuhojiwa jana na polisi, anatakiwa kuripoti tena kituoni hapo Julai 18, mwaka huu.

Akizungumzia suala la Sosopi, mwanasheria wake, Frederick Kihwelo alisema Sosopi aliripoti kituoni hapo kwani anakabiliwa na tuhuma ya kutoa lugha ya uchochezi.

Alidai lengo la mteja wake ni kuhakikisha polisi wanatenda haki bila upendeleo kwani kazi yao kubwa ni kulinda usalama wa raia na mali zao

Alisema baada ya kuhojiwa na polisi jana, atatakiwa kufika tena kituoni hapo Julai 18, mwaka huu wakati huu upelelezi unafanyika na ushahidi kupelekwa kwa Mkurugenzi wa Mashitaki ya Jinai (DPP) ili aamue kama kuna kesi ya kujibu au la.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post