Wabunge Watatu Wa CCM Wamkingia Kifua Naibu Spika Asing'oleweWABUNGE watatu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wakiongozwa na Dk Abdallah Possi ambaye ni Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge,Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu), wameutaka umma uelewe kuwa shinikizo la wapinzani bungeni kuhusu utendaji wa Naibu Spika, Dk Tulia Ackson lina uonevu wa kijinsia.


Katika mkutano huo na wanahabari uliofanyika ofisi za Waandishi wa Habari, bungeni mjini Dodoma jana, Dk Possi aliongozana na Mbunge wa Muleba Kusini, Profesa Anna Tibaijuka na Mbunge wa Sikonge, Joseph Kakunda.


Wakizungumza kwa nyakati tofauti, walisema hawakubaliani na mkakati wa kambi ya upinzani kutaka kumng’oa Naibu Spika, Dk Tulia Ackson, kwa sababu ni mkakati wenye shinikizo la kisiasa na ubaguzi dhidi ya wanawake.


Dk Possi alisema wabunge wa kambi ya upinzani hawana hoja za msingi kutaka kutekeleza mkakati wao huo kwa sababu si mara ya kwanza kwa wanaokiuka kanuni na taratibu za Bunge kutolewa au kusimamishwa.


“Tunaamini kinachotokea sasa ni msukumo wa kisiasa kwa kuwa wabunge wana njia ya kufanya kuwasilisha malalamiko yao, ikiwa wanaona wameonewa na si kupanga mkakati wa kumtoa madarakani wanayeamini anawakosea. Wana nafasi ya kukata rufaa,” alisema Dk Possi.


Profesa Tibaijuka alisema wakati Samwel Sitta akiwa Spika aliwatoa wabunge wasiofuata kanuni na hakukuwa na yanayotokea sasa, jambo linaloonesha kuwa wanamlenga Dk Tulia kwa sababu ni mwanamke.


Kakunda alisema anaamini pia kuwa maamuzi hayo ya kambi ya upinzani yana msukumo wa kisiasa kwa sababu hoja zao hazina msingi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post