Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo Acharuka Baada ya Kukabidhi Zawadi HEWA Mei Mosi


MKUU wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo ameagiza ifikapo leo, wakurugenzi wa halmashauri za mkoa huo, wawe wamewapa zawadi zao watumishi bora wa mwaka huu baada ya kubaini walitoa zawadi hewa kwenye sherehe za Mei Mosi.


Ameagiza pia Ofisi ya Katibu Tawala Mkoa wa Pwani pamoja na mkurugenzi wa Shirika la Elimu Kibaha, nao kutoa zawadi ya fedha kwa wafanyakazi waliofanya vizuri kwenye vitengo vyao, badala ya kuwapa vyeti pekee.


Akizungumza juzi kwenye sherehe za Mei Mosi zilizofanyika kimkoa wilayani Mkuranga, Ndikilo alitoa siku tatu zinazoisha leo, taasisi hizo ziwe zimetekeleza agizo hilo. Alisema walichofanya ni masihara na yeye hayuko tayari kufanyiwa mzaha katika suala hilo, lililoandaliwa kwa muda mrefu.


“Katika risala ya Shirikisho la Vyama Huru vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) Mkoa wa Pwani walilalamika kuwa kumekuwa na tabia ya baadhi ya waajiri kuwakopa zawadi za fedha watumishi wanaofanya vizuri kama motisha,” alisema.


Aliendelea, “Lakini kwa hali hii siwezi kukubaliana nalo, nawapa siku tatu muwe mmewalipa watumishi hao vinginevyo atakayeshindwa aje ofisini kwangu akutane na adhabu niliyoiandaa.”


Alisema hawezi kuvumilia watu wazembe wanaofanya dharau kwenye mambo mazito na kwamba atachukua hatua kali kwa halmashauri ambazo zitashindwa kutoa zawadi hizo kwani zingine zimetoa kwa nini wengine washindwe.


“Mimi siyo mtani wenu, wala si saizi yenu, haiwezekani mniite nije kutoa zawadi hewa, ndo maana hatua zikichukuliwa za kinidhamu mnasema mnaonewa, ikifika Jumatano muwe mmeshawapa zawadi zao wahusika, huu ni mzaha umepitiliza kiwango anayedhani tunatania aendelee aone,” alisema Ndikilo.


Licha ya ofisi ya Katibu Tawala pamoja na Shirika la Elimu Kibaha, taasisi nyingine zilizotakiwa kutekeleza agizo ni Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Halmashauri ya Mji Kibaha na Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji .


“Hatutaniani hapa,huu ni mzaha uliopitiliza kiwango,.ujumbe umefika.Namna hii mnakatisha tamaa watumishi kwa kudai kuwa mchakato bado ni jambo ambalo halijanifurahisha na nisingependa hali hii ijitokeze tena,” alisema Ndikilo.


Awali, akisoma risala ya Tucta, Amini Msambwa alisema kuwa wafanyakazi wana haki ya kutimiziwa haki zao za msingi na siyo lazima zipatikane kwa shinikizo la maandamano, migomo na hata kufungia nje waajiri.


Msambwa alisema kuwa moja ya changamoto ni baadhi ya wawekezaji wa nje na wa ndani, kuwanyima fursa wafanyakazi kujiunga na vyama vyao sehemu za kazi, ambayo ni haki yao ya kisheria na kwa kuzingatia kauli mbiu ya mwaka huu ya Dhana ya Mabadiliko ilenge kuinua hali za wafanyakazi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post