VIONGOZI WA AMCOS WANASWA NA TAKUKURU KWA MATUMIZI MABAYA YA MADARAKA
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Kigoma, inawahoji viongozi wa vyama vitatu vya ushirika vya msingi vya mazao na masoko (Amcos) mkoani humu kuhusu tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka.


Viongozi hao wanadaiwa kujikopesha Sh mil 500 kinyume na makusudio ya vyama hivyo. Hata hivyo, inaelezwa kuwa, uchunguzi utaendelea kwa vyama vingine 17 vya akiba na mikopo, ambapo viongozi wake tayari wamekwishaanza kufuatiliwa na taasisi hiyo kuhusu tuhuma mbalimbali zinazowakabili.


Mkuu wa Takukuru mkoani hapa, Mussa Misalaba, akizungumza na waandishi wa habari jana alisema, vyama hivyo vinavyotokana na wakulima wa tumbaku katika tarafa ya Nguruka wilayani Uvinza ni miongoni mwa vyama vilivyopata mkopo kutoka Benki ya CRDB, kwa ajili ya wanachama wake.


Mkopo huo kwa mujibu wa Misalaba, ulilenga kusaidia ununuzi wa pembejeo za kilimo, ujenzi wa mabani ya kukaushia tumbaku na gharama za upangaji madaraja na ununuzi wa kuni katika msimu wa kilimo wa 2015/2016.


Vyama ambavyo viongozi wake wanatuhumiwa na kuhojiwa ni pamoja na Matendo AMCOS, Sagara na Nyangabo, vyote kutoka tarafa ya Nguruka wilayani Uvinza.


Hata hivyo, Misalaba alisema baada ya kila mwanachama kuainisha kiasi alichokuwa anataka na kupatiwa mkopo huo na benki, baadhi ya viongozi na wajumbe wa bodi wa vyama hivyo, walikiuka taratibu za uendeshaji na utoaji wa mikopo hiyo, ambapo watu wachache walijikopesha fedha hizo huku idadi kubwa ya wakulima ikikosa .Inaelezwa kuwa, jambo hilo lilizua malalamiko miongo ni mwa wanachama.


Akizungumzia hali hiyo, Ofisa Tarafa ya Nguruka,Thomas Sangai alisema, kitendo cha viongozi hao kujikopesha fedha hizo, kinaathari kwa wakulima kwani wakati wa marejesho fedha hizo zitalazimika kukatwa katika mauzo ya wakulima hao.


Sambamba na hilo, imeelezwa kuwa vitendo vilivyofanywa na viongozi hao kujikopesha fedha hizo na kushindwa kuwafikia wakulima huenda vikasababisha wakulima kutorosha tumbaku na kuuza katika masoko yasiyo rasmi.


Hatua hiyo inahofiwa kuwa huenda ikachangia kupungua kwa mapato ya halmashauri, yanayotokana na ushuru wa tumbaku.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post