WAZIRI MKUU :RUSHWA INADUMAZA MAISHA YA WANANCHI




WAZIRI Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa amesema vitendo vya dhuluma, ufisadi na jeuri vinavyofanywa na watoaji na wapokeaji rushwa vinasababisha wananchi kukosa haki zao na maisha yao kuwa duni, hivyo amewataka wajumbe na Viongozi wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) kupiga vita rushwa katika ngazi zote za utawala kwenye mamlaka zao na kwa nchi.


“Sote tunakumbuka msemo wa rushwa ni adui wa haki na kwamba sitapokea wala kutoa rushwa,” amewasisitiza juu ya umuhimu wa msemo kwa sababu kuna dalili kwamba rushwa ni kikwazo kikubwa katika utekelezaji wa majukumu ya maendeleo katika ngazi mbalimbali zikiwemo za halmashauri, serikali kuu na taasisi mbalimbali za umma.


Waziri Mkuu ameyasema hayo leo mchana wakati wa ufunguzi wa mkutano mkuu wa uchaguzi wa ALAT uliofanyika mjini Dodoma ambapo amesema vitendo vya rushwa vinalalamikiwa sana na wananchi, katika maeneo yote, hususan katika huduma za afya, elimu, ardhi na utoaji leseni mbalimbali katika Serikali za Mitaa.


“Kutokana na ukweli huo, wapo wananchi ambao wameanza kupoteza imani kwa serikali yao kutokana na kuendeleza vitendo vya rushwa miongoni mwa jamii. Natoa wito kwenu mkiwa wajumbe wa chombo hiki muhimu kupiga vita vitendo vyote vinavyoashiria rushwa katika ngazi zote za utawala kwenye mamlaka zenu na kwa nchi yetu,” amesema.


Amesema hata wakati Mheshimiwa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli anazindua Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 20 Novemba, 2015 alibainisha maeneo mbalimbali ambayo ni kero kwa Wananchi mojawapo ni tatizo la rushwa miongoni mwa jamii.


Waziri Mkuu, Majaliwa amesema kuwa wakati wa kampeni za uchaguzi rais alipata fursa ya kusikiliza malalamiko mengi ya wananchi ikiwa ni pamoja na kushindwa kwa serikali za mitaa kutekeleza majukumu yake na kuwajibika kwao kama katiba, sheria na sera zinavyoelekeza.


Amesema changamoto nyingine aliyoizungumzia Mheshimiwa Rais ni upotevu wa mapato na kushindwa kukusanya kodi, ubadhirifu, matumizi mabaya ya fedha na madaraka, ambapo utekelezaji wa baadhi ya miradi upo chini ya viwango huku kukiwepo na wizi, uzembe katika mamlaka za serikali za mitaa. hivyo kusababisha upotevu mkubwa wa fedha.


Waziri Mkuu, Majaliwa amesema kuna uvujaji mkubwa wa mapato yanayokusanywa na mamlaka za serikali za mitaa kupitia mawakala au hata baadhi ya watumishi wachache wasio waaminifu, ambapo alitumia fursa hiyo kuwasisitiza usimamizi mzuri wa mapato ya halmashauri na kuhakikisha yanakusanywa kwa njia ya kielektroniki ambapo imebainika kuwa ni salama na itasaidia kupunguza kupovu huo.


“Ninatambua kwamba bado zipo changamoto za utaratibu huu wa kukusanya mapato kwa njia ya elektroniki. Aidha, zipo taarifa kuwa, baadhi ya watumishi wa halmashauri ndiyo wenye kampuni za uwakala wa kukusanya kodi na tozo mbalimbali za halmashauri, hivyo nawakumbusha watendaji wote kwamba taarifa hizi zikibainika ni za kweli, hatua za kinidhamu zitachukuliwa. Ni vyema wahusika waache tabia hiyo mara moja kwani ni kinyume na maadili ya utumishi wa umma,” amesema.


Katika hatua nyingine Waziri Mkuu, Majaliwa ameyataka mabaraza ya Madiwani yafanye kazi zake kwa mujibu wa sheria, ambapo amekemea tabia ya baadhi ya watendaji wa halmashauri kutokutaka kuulizwa chochote na mabaraza hayo kwa kisingizio kwamba wao ni watalaamu.


Amesema Mabaraza ya Madiwani ndiyo mamlaka ya wananchi katika kusimamia halmashauri hivyo kuwazuia Madiwani kuhoji chochote hata pale ambapo wataalam wamekwenda kinyume na maadili ya taaluma na utumishi wa umma siyo sahihi kiutendaji, hivyo amewataka watendaji hao kuyaachia Mabaraza hayo yafanye kazi zake na kwa mujibu wa sheria.


Kwa upande wakea Naibu Waziri wa Nchi, Osisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Suleiman Jafo amesema watahakikisha wanatoa maelekezo wanazisimamia vizuri halmashauri katika ukusanyaji wa kodi kwa mfumo wa kielektroniki.


Pia Jafo amempongeza Waziri Mkuu Majaliwa kwa utendaji wake na kwamba amewathibitishia Watanzania kuwa Rais Dk. John Magufuli hakukosea katika uteuzi huo na kwammba umakini wake katika kuchapakazi umeleta tija nchini.


Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa ALAT Taifa, Steven Muhapa akitoa hutuba ya shukurani kwa Waziri Mkuu, amesema maelekezo na maagizo yote yaliyotolewa na Waziri Mkuu wameyapokea na wataenda kuyafanyia kazi.


Imetolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post