Twaweza: Wananchi Wanaunga Mkono Haki ya Kupata Habari,Ili Kupunguza Vitendo Viovu na Rushwa


28 Aprili 2016, Dar es Salaam: 

Ingawa sheria inaipa mamlaka serikali kulifungia gazeti bila kuhojiwa, asilimia 91 ya wananchi wanasema kabla ya gazeti kufungiwa suala hilo lijadiliwe kwanza mahakamani. 



Takribani wananchi 8 kati ya 10 (78%) wanaamini upatikanaji wa habari utapunguza vitendo viovu pamoja na rushwa, huku wananchi 6 kati ya 10 (60%) wakisema serikali iwe na mamlaka tu ya kuzuia habari ambazo ni muhimu kwa usalama wa taifa. 


Hivyo basi kwa kiasi kikubwa wananchi wanaunga mkono suala la uwazi na uwajibikaji.

Matokeo haya yametolewa na Twaweza kupitia utafiti wake unaopatikana kwenye muhtasari wenye kichwa cha habari Mwangaza, Wananchi na Haki ya kupata habari.


 Muhtasari huo unatokana na takwimu zilizokusanywa kutoka kwa wahojiwa 1,811 kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania bara (Zanzibar haihusiki kwenye matokeo haya) kati ya tarehe 10 na tarehe 25 Februari 2016.

Aidha, zaidi ya nusu ya wananchi wanaamini kwamba kuna uwezekano wa kupatikana kwa taarifa muhimu kama zifuatazo:


 Namna ya kusajili uzazi (71%), namna ya kutoa taarifa juu ya kituo cha maji kilichoharibika (63%), na namna ya kutoa taarifa juu ya vitendo vya rushwa (56%). 


Hata hivyo chini ya nusu ya wananchi wanaamini wanaweza kupata taarifa kuhusu bajeti za wilaya, mipango na matumizi (42%), kiwango cha ruzuku kilichopelekwa kwenye shule zao (39%) au upungufu wa dawa kwenye vituo vya afya (35%).

Cha kushangaza ni kwamba imani hiyo haitokani na uzoefu wao kwani zaidi ya wananchi 8 kati ya 10 waliohojiwa hawajawahi kufika kwenye ofisi ya mamlaka za maji, shule za msingi za umma, vituo vya afya, wala ofisi za serikali za mitaa kutafuta taarifa zozote. 


Wananchi wengi wameonekana kutegemea zaidi redio (70%) na kwa kiwango kidogo runinga (21%) kama vyanzo vyao vikuu vya kupata habari.


 Redio inaaminika na asilimia 80 ya wananchi na runinga inaaminika na asilimia 73 ya wananchi, tofauti na magazeti yanaaminika kwa asilimia 27 tu ya wananchi. 


Japokuwa mitandao ya kijamii inaaminika kwa kiasi kidogo sana na kutumiwa kwa kiwango cha chini kama chanzo cha habari, utafiti wa Sauti za Wananchi umebaini kuwa asilimia 47 ya wananchi hutumia mitandao ya kijamii huku asilimia 53 wakiwa hawatumii. 


Bila kujali vyanzo wanavyovitumia kupata habari, wananchi bado hawapati taarifa juu ya masuala yote. Japokuwa asilimia 31 ya wananchi wamesikia kuhusu Cybercrimes Act, ni asilimia 2 pekee ya wananchi ndiyo wanaoifahamu sheria hiyo vizuri. 


Pamoja na kuwa ni moja kati ya sheria zilizojadiliwa sana na kufikishwa bungeni mwaka 2015, kiwango cha uelewa wa sheria ya Makosa ya Mtandao ni duni. Huku ukizingatia kwamba sheria hiyo inaathiri moja kwa moja haki za watumiaji wa mitandao ya kijamii.


Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, Aidan Eyakuze, anasema “Kwa kiasi kikubwa wananchi wanaunga mkono uwepo wa uwazi wa taarifa. Vilevile wameweka wazi vyanzo vya habari wanavyovitumia na kuviamini. 


Ni vema kufahamu kwamba wananchi wenye taarifa, na uhakika kwamba mawazo yao yatapokelewa, kufanyiwa kazi, na kuleta mabadiliko, wanao uwezo mkubwa wa kushiriki vizuri katika kutekeleza mipango kabambe ya serikali ya awamu ya tano”

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527