DC Afichua Siri ya Wafanya Kazi Hewa Shinyanga


Kaimu mkuu wa mkoa wa Shinyanga Josephine Matiro (pichani)ameeleza kuwa wafanyakazi hewa wengi mkoani Shinyanga wamepatikana katika sekta ya elimu kutokana na uzembe wa waratibu elimu kata na wakuu wa shule kutotoa taarifa sahihi za wafanyakazi katika maeneo yao.Matiro aliyasema hayo juzi wakati wa mkutano wa wakuu wa shule,walimu wakuu,waratibu wa elimu kata na wadau mbalimbali wa elimu kutoka halmashauri ya wilaya ya Shinyanga kilichokuwa na lengo la kufanya tathmini ya matokeo ya mtihani wa darasa la nne na saba,kidato cha pili na cha nne mwaka 2015.


Matiro ambaye ni mkuu wa wilaya ya Shinyanga alisema wafanyakazi hewa wengi Shinyanga wamepatikana katika sekta ya elimu kutokana waratibu wa elimu kutotoa taarifa sahihi za walimu huku wakuu wa shule na walimu wakuu wakikaa kimya.


“Waratibu wa elimu katika kata mnategemewa sana na halmashauri kuleta taarifa sahihi kuhusu walimu,kufuatilia shule zetu katika kata zinafanyeje,walimu wako wapi",aliongeza.


“Mnajua tumefanya suala la uhakiki,si mmesikia suala la uhakiki lilivyotusumbua Shinyanga,lakini matatizo mengi yapo kwa walimu,naomba niseme ukweli,wafanya kazi hewa wengi wako kwenye sekta ya elimu,nilichojifunza ni kwamba bado hatujatambua wajibu wetu,mwalimu mkuu upo pale,mwalimu hajaonekana mwaka mzima wala hujatoa taarifa”,alieleza Matiro.


Alisema inashangaza kuona mwalimu hayupo kazini miaka miwili lakini waratibu wa elimu,walimu wakuu na wakuu wa shule hawana taarifa na kuongeza kuwa watu hao wanatakiwa kuchukuliwa hatua kwanini hawakusema.


“Hivi inakuja akilini kweli umekabidhiwa walimu kumi,walimu wawili hawapo kwenye kituo cha kazi kwa miaka miwili au mmoja hujatoa taarifa,wewe ni kiongozi?,sasa tutawalaumu maafisa utumishi na maafisa elimu,wewe ambaye kwenye eneo lako hujasema,ina maana hujui hata walimu wako,ndiyo maana tunapata hata wafanya kazi hewa kwa sababu ya watu kutowajibika”,aliongeza Matiro.


Matiro aliwataka kuwajibika kwa nafasi zao kwani hali hiyo inasababisha baadhi ya watu kuwajibishwa kwa makosa yasiyokuwa ya kwao kutokana tu uzembe wa baadhi ya watu.


Katika hatua nyingine aliwataka wakuu wa shule na walimu wakuu kutoa taarifa sahihi kuhusu upungufu wa madawati katika shule zao na kusimamia vizuri matumizi ya pesa za ruzuku zilizotolewa na serikali huku akiwasititiza walimu kukaa karibu na wanafunzi wao na kuwafundisha madhara ya mimba na ndoa za utotoni.


Kwa upande wake mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Kiomoni Kibamba aliwataka walimu kuzingatia kanuni,sheria na maadili ya kazi yao ili kuleta mabadiliko katika sekta ya elimu.


Kibamba alisema ili kuleta uwajibikaji katika sekta ya elimu ameagiza waratibu wa elimu kata kumpelekea taarifa za vikao na shughuli wanazofanya kila mwezi katika maeneo yao na kuahidi kuwafukuza kazi walimu ambao wataonekana kuwa watoto maeneo ya kazi. 

“Mwalimu mtoro lazima tumfukuze kazi,haiwezekani hujafika shuleni siku tano bila taarifa yoyote halafu tukuache hivi hivi,hatutakubali mtu hufanyi kazi halafu unapata mshahara”,aliongeza Kibamba.Nao Maafisa elimu wa wilaya hiyo Idara ya msingi na Sekondari,Suzana Nyalubamba na Stewart Makali walisema changamoto kubwa sasa katika shule zao ni uhaba wa nyumba za walimu na kwamba wanaendelea kukabiliana na tatizo la utoro wa walimu shuleni.


Hata hivyo walisema shule za wilaya hiyo zinaendelea kufanya vizuri katika mitihani mbalimbali na wanachokisisitiza zaidi sasa ni uwajibikaji wa kila mmoja katika eneo lake.
Na Kadama Malunde-Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post