DC Shinyanga Acharuka!! Apiga Marufuku Dawa ya Mapenzi "Samba" Kwa Watoto ili Wapendwe na Wanaume Ili Kuzuia Mimba Na Ndoa za Utotoni




Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro(pichani) amepiga marufuku tabia ya wazazi kuwasafisha nyota watoto wa kike kwa kuwaogesha dawa inayojulikana kwa jina la “Samba” ili wapendwe na wanaume kwani ni kichocheo kikubwa cha mimba na ndoa za utotoni matokeo yake wanafunzi wanakatisha masomo yao shuleni.





Matiro alipiga marufuku tabia hiyo ya kuwapa dawa ya mapenzi watoto jana wakati wa maadhimisho ya tatu ya siku ya maadhimisho ya Siku ya Chama Cha Wanawake na Wasichana( Young Women's Christian Association- YWCA) duniani ambayo kwa kanda ya Ziwa Victoria yaliyofanyika katika viwanja vya Shycom mjini Shinyanga na kukutanisha wadau kutoka mikoa ya Mara,Mwanza na Shinyanga.


Kauli mbiu ya maadhimisho hayo kidunia ni "Kuunda Ulimwengu Unaojumuisha Wote" huku kauli mbiu ya maadhimisho hayo kanda ya ziwa ikiwa ni "Kwa Pamoja Tuzuie Ndoa na Mimba za Utotoni,Tutaleta Mabadiliko Kielimu".


Akizungumza katika maadhimisho hayo,Matiro ambaye ni kaimu mkuu wa mkoa wa Shinyanga alisema amepewa taarifa kuwa wazazi wengi mkoani Shinyanga wana tabia ya kuwapeleka watoto wa kike kwa waganga wa jadi kupewa “samba”(kupewa dawa ya kusafisha nyota ili wawe na mvuto kwa wanaume.


“Nitakaa na kamati ya ulinzi na usalama niagize wale waganga wote wanaosafisha nyota za watoto wa kike tuwakamate kwa sababu hatuwezi kusema tunamtetea mtoto asipate mimba wakati mtoto huyo anaenda kuogeshwa asafishe nyota,yupo darasa la tano,kwani akili yake imeshabadilishwa tayari kwamba mimi natakiwa nipendwe,natakiwa nifanyiwe hivi,je atasoma?”,alihoji Matiro.


Matiro alisema suala la ndoa na mimba za utotoni ni janga kubwa katika kanda ya ziwa hususani mkoa wa Shinyanga ambao unaongoza kitaifa kwa asilimia 59 ukifuatiwa na mkoa wa Tabora na Mara hivyo ni jukumu la kila mmoja katika jamii kuwalinda watoto.


“Naombeni mbadilike,leo wewe mzazi unafurahia kumpeleka mtoto wako asafishwe nyota ili apendwe na wanaume,akipata mimba akiwa shuleni unaanza kushangaa wakati wewe ndiyo chanzo cha matatizo”,aliongeza Matiro.


Katika hatua nyingine aliwataka wazazi kuwa karibu na watoto wao na kuwapa elimu juu ya uzazi wa mpango badala ya kuwaonea aibu matokeo yake wanajiingiza katika vitendo viovu vinavyosababisha wapate mimba na kuolewa wakiwa wadogo.


Aidha alivitaka vikundi vya akina mama katika jamii kujenga tabia ta kukutana na mabinti katika mitaa na vijiji na kuwapa elimu ya uzazi wa mpango ili kupunguza na hata kuondoa kabisa tatizo la mimba na ndoa za utotoni mkoani Shinyanga.


Kwa upande wake Katibu wa YWCA mkoa wa Shinyanga Maryciana Makundi,akisoma risala kwa mgeni rasmi ambaye ni Josephine Matiro alisema watoto wengi wa kike wanalazimishwa kuolewa kutokana na wazazi kuwa na tama ya mali,elimu duni,mfumo dume kutawala familia akidai kuwa hata kama mama hataki,hana mamlaka ya kuzuia baba asifanye atakavyo.



Makundi alisema pia watendaji katika kuwasaidia watoto kisheria huwageuka na kupkea rushwa kwa wahalifu kitendo ambacho kuwavunja moyo wahanga wa ukatili.



Aliongeza kuwa kesi nyingi za watoto waliobakwa zimekuwa zikiahirishwa kila mara licha ya kuwepo ushahidi ulio wazi dhidi ya watenda uovu na wakati mwingine kesi hazisikilizwi kabisa na zingine ushahidi hupotezwa,kukatiwa rufaa na baadhi kuzungushwa na baadhi ya wanasheria kwa maksudi yasiyokuwa ya wazi.
Na Kadama Malunde-Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527