Picha!! Mjane Wa Baba Wa Taifa, Mama Maria Nyerere Atembelea Daraja La Nyerere Kigamboni

Mke wa Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Maria Nyerere ametembelea Daraja la Nyerere linalounganisha eneo la Kigambaoni na Kurasini Jijini Dar es salaam na kuipongeza serikali na wananchi wote wa Tanzania kwa kufanikisha ujenzi wa Daraja hilo kubwa na la kisasa kwa nchi za Afrika ya Mashariki na Kati.


Mama Maria Nyerere aliyeongozana na Mwanae Mheshimiwa Makongolo Nyerere amesema kukamilika kwa daraja hilo ambalo ujenzi wake umegharimu shilingi Bilioni 254.12 kumekamilisha mpango wa miaka mingi ulioanzishwa na Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyekuwa na nia ya kujenga daraja katika eneo hilo la mkondo wa bahari lakini kwa sababu ya ufinyu wa bajeti haikuwezekana.


Aidha, Mama Maria Nyerere amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuamua Daraja hilo liitwe Daraja la Nyerere kwa heshimu ya Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, na amebainisha kuwa uamuzi huo utaviwezesha vizazi vijavyo kutambua juhudi zilizofanywa na mmewe katika ujenzi wa nchi.


"Mimi ninamshukuru sana Rais kwa maana ilikuwa lipewe jina lake, lakini yeye Mungu akamjaalia akasema kwamba hapana tukumbuke tulikotoka, kwa hiyo najisikia vizuri sana, na familia nayo inajisikia vizuri sana, lakini zaidi na watanzania wanajisikia vizuri sana, kwa maana watakuwa wanaulizana Nyerere alikuwa ni nani?" Amesisitiza Mama Maria Nyerere.


Daraja la Nyerere lenye urefu wa meta 680, upana wa meta 3.2, njia sita za magari na barabara unganishi zenye urefu wa kilometa 2.5, lilifunguliwa na Rais wa awamu ya tano Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 19 Aprili, 2016 na linakuwa kiunganishi muhimu kati ya Kigamboni na katikati ya Jiji la Dar es salaam.


Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
27 Aprili, 2016



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527