Makonda : Ombaomba Dar Ni Mawakala Wa Kusambaza Dawa za Kulevya



Mkuu wa Mkoa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema kwa mujibu wa utafiti alioufanya, ombaomba walioko jijini Dar es Salaam baadhi yao wanajihusisha na uuzaji wa dawa za kulevya.


Akihojiwa katika mahojiano ya moja kwa moja na kituo kimoja cha redio, Makonda alisema wapo watu ambao wanatumia mwanya huo kusambaza dawa za kulevya.


“Wapo wanaotumia fursa hii kusambaza dawa za kulevya kwa sababu anavyopita huwezi kumhisi kwa namna anavyoonekana, lakini watu hawa ni miongoni mwa mawakala wa kusambaza dawa za kulevya,” alisema Makonda.


Makonda aliwataka wakazi wa jiji hilo kushirikiana naye katika kuwaondoa ombaomba hao ambao wengi wanatoka nje ya Da es Salaam na kwamba hakuna tija kuendelea kuwaacha.


“Watanzania tuna upendo sana lakini tunahitaji kutafakari kama kweli watu walioko barabarani wakiomba kama kweli wanahitaji msaada huo au la,” alisema Makonda.


Alisema kwa kuendelea kuwaacha ombaomba hao pia kutasababisha vijana ambao sasa wanaomba barabarani kuwa watu hatari katika maisha yao ya baadaye kwani wakikosa pesa wataingia katika shughuli za uporaji ili wapate fedha.


“Itafika kipindi ataanza kuangalia kile alichokuwa anakikusanya wakati akiomba na kile anachokipata akifanya kazi, ataona akifanya kazi hapati kiasi kikubwa, ataamua kuwa mporaji,” alisema Makonda.


Makonda alisema kwa mujibu wa utafiti alioufanya, asilimia 80 ya ombaomba wanatoka nje ya Dar es Salaam na kesho operesheni ya kuwaondoa watu hao itaanza rasmi huku wale ambao hawana ulemavu wowote wakikamatwa kwa makosa ya uzururaji.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post