
Mkuu
wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro amemsweka rumande Muhandisi wa
halmashauri ya manispaa ya Shinyanga Simoni Ngagani, baada ya kupuuza
agizo lake la kufanya maandalizi mapema ya kununua kokoto na Saruji kwa
ajili ya kusimika mapipa 50 ya kutunzia uchafu kwenye mitaa mbalimbali
katika manispaa ya Shinyanga ikiwemo eneo la kituo cha mabasi yaendayo
wilayani.
Tukio hilo limetokea jana asubuhi mjini Shinyanga wakati mkuu huyo wa wilaya akiwa na msafara wake alipowasili katika eneo la stendi ya mabasi yaendayo wilayani kwa lengo la kufanya uzinduzi wa kusimikwa kwa mapipa hayo na kukuta maandalizi hayajakamilika.
Matiro
alimuagiza Mhandisi huyo kufanya maandalizi hayo mapema mbele ya
mkurugenzi wake wa manispaa ya Shinyanga Kalinjuna Lewis, kuwa ataandaa
vifaa hivyo majira ya saa moja asubuhi ili zoezi la kusimika mapipa
hayo likamilike haraka, na baada ya hapo wafanye usafi wa mazingira
lakini agizo hilo lilipuuzwa na mhandisi huyo .
Mkuu
huyo alipomhoji mhandisi kwanini alipuuzia agizo lake la kufanya
maandalizi mapema, mhandisi huyo alisema sababu iliyomkwamisha ni
kukosekana kwa pesa za kununua kokoto na saruji kwani mvua kubwa
ilinyesha na kushindwa kwenda benki, na alivyoamka asubuhi ndipo
atakafuta dhana hizo.
Hata
hivyo mkuu huyo hakuridhika na majibu hayo ndipo DC alipochukua uamuzi
ya kumsweka rumande kwa kumuagiza mkuu wa kituo cha polisi wilaya ya
Shinyanga kumkamata na kumuweka ndani mhandisi huyo wa ujenzi manispaa
hiyo Samson Ngagani kwa kosa la kuchelewesha maandalizi ya vifaa vya
ujenzi vilivyopangwa kutumika kusimika mapipa ya taka.
“Haiwezekani
tukubaliane tuamke mapema ili tufanye kazi hii haraka na pia tuingie
Mitaani kufanya usafi, ambapo mimi nimeamka saa 11 nikajiandaa harafu
wewe una kuja saa mbili tena bila ya kufanya maandalizi yeyote hii ni
kunidharau, hivyo naagiza OCD mkamate akakae Rumande kwanza ili liwe
fundisho kwa wengine” ,alisema Matiro.
Katika
uzinduzi huo Matiro alisema mapipa hayo ya taka ambayo idadi yake ni
zaidi ya 50 yatawekwa katika maeneo mbali mbali ya manispaa ya Shinyanga
na wananchi wanatakiwa kuyalinda.
Awali
akiongea katika uzinduzi huo, mkurugenzi wa manispaa ya Shinyanga Lewis
Kalinjuna alisema mapipa hayo yamepatikana kutokana na wadau mbali
mbali kujitolea kuchangia baada ya kuhamasishwa na mkuu huyo wa wilaya
ambapo pipa moja limegharimu shilingi elfu 90.
Naye
afisa afya wa manispaa ya shinyanga Elly Nakuzelwa alisema lengo la
kuweka mapipa hayo ya taka ni kuhakikisha manispaa ya Shinyanga inakuwa
katika hali ya usafi ili kuondoa magonjwa ya miripuko yanayosababishwa
na uchafu ikiwemo kipindupindu.
Habari na Marco Maduhu na Veronica Natalis-Malunde1 blog
Angalia hapa chini picha yaliyojiri katika uzinduzi huo

Wa kwanza kulia ni Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akimhoji Mhandisi wa ujenzi wa manispaa ya Shinyanga Simon Ngagani (katikati mwenye kaunda suti)kwa kupuunza agizo lake la kufanya maandalizi mapema ya kununua vifaa vya ujenzi vya kusimikia Mapipa ya uchafu 50 katika mitaa mbalimbali ya Mji wa Shinyanga ,na mwenye traksuti kushoto ni Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Kalinjuna Lewis akishuhudia Mtumishi wake akikamuliwa Jipu na hatimaye kuswekwa rumande kwa kumpuuza DC huyo-Picha zote na Marco Maduhu-Malunde1 blog

Mhandisi wa manispaa ya Shinyanga Simon Ngagani akijitetea kwa mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro(kulia),kushoto ni mkurugenzi wa manispaa ya Shinyanga Lewis Kalinjuna akisikiliza utetezi wa mhandisi wake japo aliambulia kuwekwa rumande

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akiongea na wananchi kabla ya kuanza zoezi la kusimika mapipa hayo ya uchafu huku akiwaasa wayahifadhi na kutoyauza kama vyuma chakafu.

Mwananchi akila Miguu ya kuku kwenye zoezi la kusimika mapipa hayo huku mkuu wa wilaya ya Shinyanga akitoa elimu ya kuhifadhi mazingira kwa kutumia mapipa hayo ya uchafu

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akishiriki zoezi la kusimika mapipa hayo ya uchafu

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akichanganya zege kwa ajili ya kusimika mapipa ya uchafu

![]() |
Kushoto ni Meneja wa benki ya CRDB tawi la Shinyanga Said Pamui,ambaye ni miongoni mwa wadau waliochangia mapipa hayo akishiriki zoezi la kusimika mapipa,aliyeshikilia koleo kulia ni mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro |
![]() |
Meneja wa benki ya CRDB tawi la Shinyanga Said Pamui,ambaye ni miongoni mwa wadau waliochangia mapipa hayo akishiriki zoezi la kusimika mapipa |

Baada ya kumaliza kuzindua zoezi la kusimika Mapipa ya uchafu, Mkuu huyo wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro alianza kukagua Mazingira ya eneo la stendi ya Mabasi ya kwenda wilayani na kukuta hali mbaya ya uchafu ,huku choo cha standi hiyo kikitisha kwa uchafu kama unavyoona kwenye picha hapo juu na hapa chini,ambapo chemba za vyoo zimeziba kwa vinyesi, hali ambayo ilimfanya mkuu huyo wa wilaya kumuagiza Mkurugenzi afanye usafi haraka ndani ya wiki moja akute pasafi

Choo cha stendi ya mabasi yaendayo wilayani kikiwa kimezungukwa na uchafu yakiwemo maji machafu yaliyotuama,pichani ni afisa mazingira wa manispaa ya Shinyanga Elly Nakuzelwa akiingia katika choo hicho

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga akishuhudia uchafu katika eneo la stendi ya mabasi yaendayo wilayani mjini Shinyanga

Uchafu ukiwa katika choo cha stendi hiyo

Chemba ya choo ikiwa imeziba
Picha zote na Marco Maduhu-Malunde1 blog