CHINA YASEMA UCHAGUZI WA ZANZIBARI ULIKUWA HURU NA HAKI


Balozi wa China nchini Tanzania Dkt. LU Youqing amefanya mazungumzo na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais – Muungano na Mazingira Mh. January Makamba Ofisini kwa Waziri huyo Mtaa wa Luthuli jijini Dar es Salaam.


Katika mazungumzo yao Balozi wa China amesema kuwa Serikali ya China inaamini kwamba uchaguzi wa Zanzibar uliofanyika mwishoni wa wiki iliyopita ulikuwa huru na haki.


Balozi Youqing amesema kuwa Makamu wa Rais wa China ametuma salamu za pongezi kwa Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein kwa kuchaguliwa kwake na kwa watu wa Zanzibar kwa kuendesha uchaguzi huo katika misingi ya haki na uhuru.


“Alikuwepo shuhuda wetu katika kushuhudia uchaguzi huo na alituambia kuwa ulikuwa wa haki na uhuru,” alisema Balozi huyo.


Katika mazungumzo hayo Balozi Youqing alisema Serikali ya China itaendelea kutoa misaada na kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwani huo ni wajibu wa mataifa makubwa kwa nchi zinazoendelea.


Alimhakikishia Mheshimiwa Makamba kwamba China ina mipango mingi ya ushirikiano na Tanzania, ikiwemo kwenye sekta ya umeme na itaendelea kutoa ushirikiano kwa Tanzania, ikiwemo kupitia makampuni ya China, ili kuhakikisha malengo ya Tanzania kwenye sekta ya umeme yanatimia.


Kwa upande wake, Mheshimiwa Makamba alimshukuru Balozi Youqing pamoja na Serikali ya China kwa ushirikiano uliopo baina ya nchi hizo mbili.


“Ujumbe na salamu ulizotoa leo umetupa faraja Watanzania. Urafiki baina ya nchi zetu, na baina ya vyama vyetu vya CCM na CCP, ni wa muda mrefu, ni wa majira yote, na umejengwa kwenye misingi ya kuheshimiana na hauna budi kuendelezwa”, alisema Mheshimiwa Makamba.


Pia Waziri Makamba na Balozi Youqing walikubaliana kutembelea Pemba na Unguja kwa pamoja mwezi Aprili ili kukagua na kutengeneza miradi ya maendeleo kati ya China na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.


Vilevile, walikubaliana kuhusu kutengeneza mradi mkubwa wa ushirikiano kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muugano wa Tanzania na China kwenye teknolojia zitakazosaidia kupunguza matumizi ya mkaa, hivyo kuhifadhi mazingira.


Waziri Makamba pia amemueleza Balozi Youqing kuhusu hitaji na umuhimu wa ushirikiano katika kuiwezesha Tanzania kumiliki teknolojia ya uzalishaji wa nishati kwa kutumia taka ngumu zinazozagaa katika miji ya Tanzania ambapo Balozi Youqing aliahidi kulifuatilia suala hilo.


IMETOLEWA NA:
KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI,
OFISI YA MAKAMU WA RAIS.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527