MWAKYEMBE APOKEA TAARIFA YA SHERIA YA MANUNUZI YA UMMA


Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt.Harrison Mwakyembe amepokea taarifa ya utafiti wa marekebisho ya Sheria ya Manunuzi ya Umma kutoka Tume ya kurekebisha Sheria.


Akipokea taarifa hiyo jana Jijini Dar es salaam Mhe. Dkt.Harrison Mwakyembe alisema taarifa hiyo ya utafiti itasaidia kurekebisha sheria ya manunuzi ambayo inalenga kukuza uchumi wa nchi.


“Mimi na wataalamu wangu tumeipokea taarifa hii, tutaiangalia na kuhakikisha tunaifikisha Wizara ya Fedha na Mipango na kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili kuendelea na utaratibu unaofuata ili mchakato wa marekebisho uweze kufanyika kwa haraka”alisema Dkt Mwakyembe.

Akifafanua juu ya sheria ya manunuzi ya Umma, Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebisha Sheria Jaji Aloysius Mujulizi amesema kuwa Tume imefanya utafiti wa sheria hiyo kwa kushirikisha wadau mbalimbali.


“Tumepata maoni mengi na ushirikiano mkubwa kutoka kwa viongozi na wasimamizi wa manunuzi ya Serikali kwa namna wanavyoiona sheria ya manunuzi ya Umma,na sisi tumeyachambua maoni hayo kwa kutumia vigezo vya sheria”alisema Jaji Mujulizi.


Aidha,Tume imetoa maoni kwa Serikali kusimamia sheria ili iweze kuendana na ukuaji wa uchumi nchini kwa kurekebisha baadhi ya sheria ili kuepuka muingiliano uliopo kati ya sheria ya manunuzi na sheria nyingine.


Marekebisho ya sheria hii ni moja ya agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt. John Pombe Magufuli lililotolewa Novemba 2015 alipokua akizindua Bunge la 11.

Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebisha Sheria Jaji Aloysius Mujulizi (Kushoto) akizungumza wakati wa kuwasilisha taarifa ya utafiti wa marekebisho ya Sheria ya Manunuzi ya Umma, katikati ni Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt.Harrison Mwakyembe na kulia ni katibu Mkuu wa Wizara hiyo Prof. Sifuni Mchome.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527