BOMBA LA MAFUTA MAZITO KUTOKA UGANDA LITAJENGWA KUPITIA ARDHI YA TANZANIA KWENDA TANGA


KAMPUNI ya Total E&P Uganda imesisitiza kwamba bomba la mafuta mazito kutoka Uganda, litajengwa kupitia ardhi ya Tanzania kwenda Bandari ya Tanga, licha ya kuwepo kwa mazungumzo ya kushawishi lipite katika ardhi ya Kenya kwenda Bandari ya Lamu, ambayo haijajengwa.


Gazeti la Kenya la Daily Nation liliweka taarifa hiyo jana katika mtandao wake, ikimnukuu Meneja Mkuu wa kampuni hiyo, Adewale Fayemi akisema njia hiyo ni nafuu kwao.


“Msimamo wa kampuni yetu umebakia kuwa bomba litakwenda Bandari ya Tanga, naelewa kuna mambo yanaendelea kujadiliwa lakini msimamo wetu umebaki pale pale,” amekaririwa Fayemi na gazeti la Daily Nation.


Fayemi amekaririwa akisema kabla ya kufikia uamuzi wa kupeleka bomba hilo kwenda Bandari ya Tanga, walifanya tathimini na kuangalia fursa zote.


Katibu Mkuu wa Nishati wa Kenya, Joseph Njoroge, alipohojiwa amekaririwa akisema kama nchi yake ikikosa fursa ya kupitisha bomba hilo katika ardhi yake, Kenya itajenga bomba lingine bila kujali kama itapata ushirikiano na Uganda au la.


Bomba hilo kupita katika ardhi ya Tanzania kwenda Bandari ya Tanga, kuna unafuu mkubwa na utekelezaji wake utakuwa na ufanisi kutokana na kutokuwepo tishio la ulinzi na usalama wa miundombinu kama ilivyo Kenya.


Mbali na unafuu na kutokuwa na tishio la usalama,Tanzania ndiyo yenye uzoefu wa muda mrefu na wa hivi karibuni wa ujenzi, uendeshaji, ulinzi na uelimishaji jamii katika miradi ya bomba la mafuta.


Uzoefu huo unatajwa kuwa ni wa ujenzi, uendeshaji na uhudumiaji wa Bomba la Mafuta la Tanzania na Zambia (Tazama) tangu mwaka 1968, likitoka Dar es Salaam mpaka Ndola Zambia. Bomba hilo lenye kipenyo cha nchi 8 mpaka 12 na urefu wa kilometa 1,710; kati ya hizo kilometa 860 zipo kwenye ardhi ya Tanzania na limekuwa likipitisha mafuta tani milioni 1.1 kwa mwaka.


Tanzania pia ina sifa ya uzoefu wa ujenzi, uendeshaji na uhudumiaji wa bomba la gesi kutoka Songo Songo mpaka Dar es Salaam, lenye kipenyo cha nchi 12 na urefu wa kilometa 25 kutoka kisiwa cha Songo Songo mpaka Somangafungu.


Pia kuna bomba lingine la urefu wa kilometa 207 na kipenyo cha nchi 16, kutoka Somangafungu mpaka Ubungo Dar es Salaam, mbali na bomba kubwa la gesi kutoka Mtwara mpaka Kinyerezi Dar es Salaam lenye zaidi ya kilometa 490.


Lipo pia bomba la gesi linalotoka Mnazi Bay kwenda Mtwara, urefu wa kilometa 27 na kipenyo cha nchi 8, ambalo limeanza kutumika tangu 2006.


Akizungumza hivi karibuni katika mahojiano na Shirika la Utangazaji (TBC), Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC), Dk James Mataragio, alisema bomba hilo likipita Tanzania kwenda Tanga, kampuni hiyo ya Total itapata nafuu ya Dola za Marekani milioni 500, sawa na zaidi ya Sh trilioni moja za Tanzania.


Aliwataka Watanzania kila mmoja kwa nafasi yake kushawishi na kuvutia mradi huo, kwa kuwa una faida za ziada zitakazoendana na mradi huo, ikiwemo kuongezeka kwa wawekezaji na kujenga miundombinu ya mawasiliano sambamba na bomba hilo.


Bandari ya Tanga iko tayari na ina mazingira wezeshi ya asili ikiwemo kina kirefu kinachoruhusu meli kubwa kufunga gati bila usumbufu na kingo za asili, wakati Kenya bandari inayokusudiwa ya Lamu haijajengwa.


Mpaka sasa,bandari ya Tanga imeshakamilisha Tathimini ya Athari za Kimazingira (EIA) na Upembuzi Yakinifu, wakati njia ya Tanga ya bomba hilo imekwishaainishwa na haitapitia katika hifadhi za taifa wala mapori ya akiba.


Bandari ya Tanga pia inayo fursa ya kutumika zaidi na mradi huo, kwa kuwa haina msongamano wa shughuli za bandari na tayari Serikali ya Tanzania kupitia Mamlaka ya Bandari (TPA), imeshatenga fedha za upanuzi utakaohitajika na eneo.


Bandari hiyo pia imeunganishwa kwa reli na barabara za lami, zinazokwenda nchi za jirani na hivyo iko tayari kuanza kutumika kwa ajili ya kuingizia mizigo kwa ajili ya ujenzi wa mradi huo.


Bomba hilo litakuwa na urefu wa kilometa 1,410 na litasafirisha mafuta ghafi mapipa 200,000 kwa siku kutoka Ziwa Albert nchini Uganda, hadi Bandari ya Tanga na ujenzi wake unatarajiwa kuzalisha ajira za moja kwa moja 1,500 na ajira zisizo za moja kwa moja 20,000.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527