Bandari Ya Dar es Salaam Kuunganisha Singapore Na Afrika Mashariki


Waziri wa Biashara na Viwanda wa Singapore, Dk. Koh Poh Koon, amesema wamepanga kutumia bandari ya Dar es Salaam kuwa kiunganishi cha biashara kati ya nchi hiyo na mataifa mengine ya Afrika Mashariki.


Dk. Koon ameyasema hayo jana(Jumatano, Aprili 27, 2016), wakati alipomtembelea Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ofisini kwake mjini Dodoma, na kwamba Singapore ipo tayari kutoa fursa kwa wataalam wa Tanzania kwenda kufanya kazi katika Bandari ya Singapore ili kupata uzoefu utakaosaidia uendeshaji wa bandari za Tanzania.


Dk. Koon ambaye ameambatana na wafanyabiashara wakubwa wapatao 40, amemweleza Waziri Mkuu kwamba kampuni ya Hyflux ya Singapore imeanza kuwekeza nchini kwa kujenga eneo maalum la uchumi (Special Economic Zone) mkoani Morogoro ambapo ndani ya kipindi cha miaka mitano wanatarajia kujenga miundombinu wezeshi ya kuweka viwanda vya kati (light industries), maeneo ya biashara na nyumba za makazi zipatazo 37,000.


“Jiwe la msingi la mradi huo litawekwa tarehe 29 Aprili 2016 na Waziri wa Biashara,Viwanda na Uwekezaji, Charles Mwijage,” alisema.


Mbali na ushirikiano katika sekta ya biashara na uwekezaji, Dk Koon amweleza Waziri Mkuu kwamba nchi yake itaisaidia Tanzania kujenga uwezo wa kiufundi katika maeneo mbalimbali ya menejimenti na uendeshaji wa bandari na ufundi katika sekta ya gesi na mafuta.


“Hadi sasa makampuni ya Singapore yaliyowekeza nchini ni pamoja na Pavillion Energy ambayo imewekeza kiasi cha Dola za Kimarekani bilioni 1.2 katika sekta ya gesi na inatarajia kuwekeza zaidi dola za kimarekani bilioni 3 kwa ajili ya ujenzi wa kinu cha kuchakata gesi (LNG plant) kitakachojengwa mikoa ya Kusini kwa ubia na makampuni ya gesi kutoka Ulaya na Marekani”.


Amesema kampuni ya PIL ya Singapore inatarajia kuwekeza Dola za Kimarekani milioni 400 kwa ajili ya kuanzisha kituo cha kutoa huduma kwa makampuni ya gesi.


Amesema lengo la ziara hiyo ni kuimarisha ushirikiano baina ya mataifa hayo pamoja na kuweka mikakati ya kuinua uchumi na kupanua wigo wa biashara.


Kwa upande wake, Waziri Mkuu Majaliwa ameishukuru Serikali ya Singapore kwa uwekezaji unaofanywa na makampuni yake nchini na kwa misaada ya kiufundi ambayo wameitoa kwa Tanzania katika nyanja mbalimbali.


Ili kusaidia juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano za kukuza uchumi, Waziri Mkuu ameyakaribisha makampuni mengine ya Singapore kuja nchini kufanya uwekezaji katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuanzisha viwanda, mahoteli, kilimo na nishati.


Amemuahidi Dk. Koon kwamba Tanzania ipo tayari kukamilisha mazungumzo ya kusaini Mkataba wa Kuvutia na kulinda uwekezaji baina ya nchi mbili (Bilateral Investment Protection and Promotion Agreement) na Mkataba wa Kuepuka kutoza ushuru mara mbili (Double Taxation Avoidance Agreement) ili kuvutia uwekezaji zaidi kutoka Singapore.


Waziri Mkuu, Majaliwa amewataka Watanzania kutumia fursa ya ushirikiano kati ya Singapore na Tanzania kuanzisha biashara mpya zitakazowanufaisha wote.


Waziri Mkuu amesema Singapore ina uwezo mkubwa kibiashara pamoja na uzoefu wa siku nyingi kwenye uendeshaji wa bandari hivyo Tanzania itapata nafasi ya kujifunza namna ya uendeshaji katika sekta hizo.


Amesema Tanzania imefungua milango ya uwekezaji kwa wafanyabiashara wa Singapore kuja kuwekeza katika sekta za viwanda, usafiri wa anga na kwenye Maeneo ya Uzalishaji kwa Mauzo Nje (EPZ).

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527