Angalia Picha-Rais Magufuli Aongoza Waombolezaji Kuaga Mwili Wa Mbunge Christina Lissu Jijini Dar Leo


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 12 Aprili, 2016 ameungana na Ndugu, Jamaa na Marafiki kuuaga mwili wa Mbunge Mstaafu wa Mkoa wa Singida Marehemu Christina Lissu Mughwai katika ukumbi wa Karimjee, Jijini Dar es salaam.

Christina Lissu Mughwai aliyekuwa Mbunge wa viti Maalum Mkoa wa Singida katika kipindi cha kuanzia mwaka 2010 hadi 2015, alifariki dunia tarehe 07 Aprili, 2016 katika hospitali ya Agha Khan Jijini Dar es salaam, alikokuwa akipatiwa Matibabu.

Pamoja na Rais Magufuli na Mkewe Mama Janeth Magufuli, Viongozi wengine waliohudhuria shughuli ya kuaga mwili wa Marehemu Christina Lissu Mughwai ni Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Tulia Akson na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bunge Mheshimiwa Freeman Mbowe.

Akitoa salamu kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mheshimiwa George Simbachawene amewapa pole familia ya marehemu na kueleza kuwa katika kipindi chake cha ubunge Mheshimiwa Christina Lissu Mughwai alitoa mkubwa kama mbunge na kama mtaalamu wa Uchumi.

"Mheshimiwa Rais anatoa pole nyingine kwenu familia ya marehemu, ndugu jamaa na marafiki wote walioguswa na msiba huu. Bwana alitoa na Bwana ametwaa, jina lake lihimidiwe, Amina" Amesema Mheshimiwa Simbachawene.

Mwili wa Marehemu Christina Lissu Mughwai umesafirishwa leo kwenda kijiji cha Mahambe Mkoani Singida kwa Mazishi.

Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
12 April, 2016



Rais wa Jamhuri ya Muungano Dkt. John Pombe Magufuli akimfariji Mwanasheria Tundu Lissu (Mb) kufatia kifo cha mdogo wake Christina Lissu Mughwai aliyefariki Aprili 7 mwaka huu.

Mke wa Rais Mama Janeth Magufuli akimpa pole Mwanasheria Tundu Lissu (Mb) kufatia kifo cha mdogo wake Christina Lissu Mughwai aliyefariki Aprili 7 mwaka huu

Rais wa Jamhuri ya Muungano Dkt. John Pombe Magufuli akiteta jambo na mwenyekiti wa chama cha CHADEMA Freeman Mboye wakati wa akiaga mwili wa marehemu Christina Lissu Mughwai aliyewahi kuwa Mbunge wa Viti Maalum kutoka Chadema katika ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam.


Rais wa Jamhuri ya Muungano Dkt. John Pombe Magufuli na mke wake mama Janeth Magufuli wakiaga mwili wa marehemu Christina Lissu Mughwai aliyewahi kuwa Mbunge wa Viti Maalum kutoka Chadema katika ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post