RAIS MAGUFULI ABAINI MADUDU BENKI KUU YA TANZANIA (BOT), AMEFANYA MAAMUZI HAYA



TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amefanya ziara ya kushitukiza katika Benki Kuu ya Tanzania (BOT), ambapo pamoja na mambo mengine ameiagiza Benki hiyo kusitisha mara moja ulipaji wa malimbikizo ya malipo ambayo tayari yalishaidhinishwa (Ex-Checker) na badala yake yarejeshwe Wizara ya fedha na Mipango kwa ajili ya kufanyiwa uhakiki.


Mpaka Rais Magufuli anatoa agizo hilo, Benki Kuu ya Tanzania ilikuwa katika mchakato wa kufanya malipo ya shilingi Bilioni 925.6, ambazo Wizara ya Fedha ilitoa idhini ya kufanyika malipo.


Akizungumza na watendaji wakuu wa Benki Kuu ya Tanzania waliojumuisha Gavana, Naibu Magavana, Wakurugenzi na Mameneja, Rais Magufuli ametaka Wizara ya Fedha ifanye upya uhakiki wa malipo hayo, ili kubaini kama walengwa walioidhinishwa kulipwa wanastahili kulipwa ama vinginevyo.


Aidha, Dkt. Magufuli ameagiza Kitengo cha madeni ya nje ambacho awali kilikuwa chini ya Benki Kuu na baadaye kikahamishiwa Wizara ya Fedha, kirejeshwe Benki Kuu mara moja ili kuimarisha udhibiti wa ukopaji na ulipaji wa madeni.


Wakati huo huo, Rais Dkt. John Pombe Magufuli amemuagiza Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania Prof. Beno Ndulu kupitia upya orodha ya wafanyakazi wa Benki hiyo, na kuwaondoa mara moja wale wote ambao hawana ulazima wa kuwa wafanyakazi katika benki hiyo.


"Haiwezekani tukawa na kundi kubwa la wafanyakazi, wanalipwa mishahara wakati hata kazi wanazofanya hazijulikani" Amesema Dkt. Magufuli.

Rais Magufuli ametoa agizo hilo wakati ambapo Benki Kuu ya Tanzania ina wafanyakazi 1391.


Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam-10 Machi, 2016.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli akiwa kaongozana na Naibu Gavana wa BOT Dkt Natu Mwamba akiwasili makao makuu ya Benki Kuu ya Tanzania alikofanya ziara ya kushtukiza leo Machi 10, 2016.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na ungozi wa juu wa Benki Kuu ya Tanzania ambao ameupa maelekezo mbalimbali katika kuboresha utendaji wao wa kazi wakila siku.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akikagua CV za wafanyakazi wa Benki Kuu ya Tanzania wakati wa ziara yake ya kushtukiza jijini Dar es Salaam. Kulia kwake ni Gavana wa Benki Kuu Beno Ndulu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527