MLINZI WA HOTELI AWATANDIKA RISASI MADEREVA WA MALORI BAADA YA MMOJA WAO KULETA UBISHI


Madereva watatu wa malori yaendayo mikoani na wasaidizi wao watatu, wamenusurika kifo baada ya kupigwa risasi sehemu mbalimbali za mwilini na mlinzi wa nyumba moja ya wageni iliyopo Ubena, Chalinze mkoani Pwani.


Tukio hilo limetokea jana alfajiri saa 11.30 kwenye hoteli hiyo ambako madereva na wasaidizi hao walikuwa wamefikia kwa mapumziko kabla ya kuendelea na safari.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Boniventura Mushongi alisema tukio hilo lilitokea baada ya kuwapo kutokuelewana kati ya mmoja wa madereva na mlinzi wa nyumba hiyo.


Kamanda Mushongi alisema taarifa za awali zinasema baada ya mabishano hayo ambayo bado hayajajulikana chanzo chake, mlinzi huyo alikoki silaha yake aina ya Shortgun na kupiga risasi moja hewani kutuliza vurugu na kumjeruhi mmoja wa madereva hao.


Hata hivyo, mabishano yalizidi baada ya madereva wengine kujitokeza kuingilia ndipo mlinzi huyo akapiga risasi nyingine ambayo ilitoka na gololi zake kusambaa na kuwajeruhi wengine wanne ambao walipelekwa Kituo cha Afya Chalinze kwa matibabu.


Alisema mlinzi huyo amekimbia na anaendelea kutafutwa na chanzo cha tukio hilo kinachunguzwa.


Mganga Mkuu wa Hospitali ya Chalinze, Dk Victor Bamba alisema walipokea majeruhi watano ambao walipatiwa huduma ya kwanza na kutokana na hali zao kuwa mbaya walihamishiwa Hospitali ya Tumbi.


Akizungumza wodini Tumbi walikolazwa, mmoja wa madereva hao, Harun Adeli alisema walifika hapo juzi saa mbili usiku na kuamua kulala ndani ya magari yao ili jana waendelee na safari na ilipofika saa kumi na moja alfajiri walisikia makelele yanayoashiria ugomvi ndani ya hoteli hiyo.


“Wakati tunashangaa tulishtukia risasi zinarindima na ndipo zilipotufikia,” alisema.


Muuguzi wa zamu katika Hospitali ya Tumbi, Habibu Yahaya alisema aliwapokea majeruhi Stephen Fredy, Beno Henry, Akrey Dallu, Ramadhani Saidi, Amani Almasi na Adel wote wakazi wa Dar es Salaam.


Diwani wa Ubena, Nicolaus Muyunga alisema kwa mujibu wa majirani, yalitokea mabishano kati ya utingo na dereva ambao walikuwa wamekunywa na kulala kwenye meza muda mrefu, walipotakiwa kuchukua vyumba wakalale ndani au warudi katika magari yao walikataa na mlinzi alipotaka kuwaondoa kwa nguvu walimzidi nguvu, hivyo akajitetea kwa kupiga risasi hewani.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527