JINSI LOWASSA ANAVYOIPASUA CCM



Uamuzi wa Edward Lowassa kujiondoa CCM na kujiunga Chadema, bado unakitesa chama hicho tawala baada ya mikoa kuanza kuwashughulikia viongozi waliomuunga mkono wakati wa Uchaguzi Mkuu, huku baadhi wakisema wako tayari kupambana na wanaowatuhumu kusaliti chama.


Lowassa alijiengua CCM Julai mwaka jana baada ya jina lake kuondolewa kwenye mbio za urais kwa tiketi ya chama hicho, na baadaye kufuatwa na mawaziri, wabunge, wenyeviti wa mikoa na madiwani na hivyo kufanya Uchaguzi Mkuu kuwa na ushindani mkubwa.


Baada ya kumalizika kwa uchaguzi huo, viongozi na wanachama wa CCM walioonekana kuwa karibu na waziri huyo mkuu wa zamani, walituhumiwa kukihujumu chama kwa kumpigia kampeni Lowassa wakati wa usiku, huku mchana wakijionyesha kuwa wanaunga mkono wagombea wa CCM.


Tuhuma hizo ziliongezewa nguvu na mwenyekiti wa CCM, Jakaya Kikwete takriban wiki mbili zilizopita alipotangazakuwa waliosaliti chama hicho watatumbuliwa bila ya aibu, na tayari mkoa wa Manyara umeshatangaza kuwatimua uanachama viongozi 21 wanaotuhumiwa kushabikia upinzani.


Viongozi wa mikoa wamekanusha tuhuma zinazoelekezwa kwao kuwa walisaidia upinzani wakati wa uchaguzi wa mwaka jana.


Miongoni mwa wanaotuhumiwa ni mwenyekiti wa Mkoa wa Iringa, Jesca Msambatavangu ambaye aliangushwa kwenye kura za maoni ndani ya chama hicho na Frederick Mwakalebela, ambaye pia alishindwa na Mchungaji Peter Msigwa kwenye kinyang’anyiro cha ubunge wa Jimbo la Iringa Mjini.


Mwenyekiti huyo anatuhumiwa kubadili timu yake ya kampeni na kuifanya iwe ya kumpigia debe mgombea huyo wa Chadema.


Lakini Msambatavangu, ambaye pia anadaiwa kutoa gari zake zitumike kwenye kampeni za wapinzani, alisema yupo tayari kuhojiwa ili ajibu tuhuma dhidi yake ambazo tayari zimewasilishwa kwenye chama hicho.


Alisema anasubiri ahojiwe ili aeleze ukweli kuhusu suala hilo.
Mwakalebela alifungua kesi Mahakama Kuu akidai kuwa taratibu zilikiukwa wakati wa kuhesabu kura.


Mwingine anayezungumzwa ni mwenyekiti wa CCM wa Simiyu, Dk Titus Kamani, ambaye alikuwa Waziri wa Uvuvi na Maendeleo ya Mifugo katika Serikali iliyopita, ambaye amezielezea tuhuma dhidi yake kuwa ni majungu ya wasiompenda ambao wanataka avuliwe uongozi.


Dk Kamani anadaiwa kuwawezesha kwa hali na mali baadhi ya wagombea wa upinzani, kama kutoa vyombo vya matangazo na gari lake wakati wa kampeni.


Ilidaiwa kuwa kutokana na msaada huo, wagombea wa upinzani walishinda katika kata ya Lamadi na Mkula.


“Matokeo ya uchaguzi yanaonyesha wazi kuwa wanaCCM kwa ujumla walikuwa na umoja,” alisema Dk Kamani.


“Majimbo mawili kati ya saba kwenye mkoa huu yalikuwa yanashikiliwa na upinzani, lakini tumefanikiwa kuyakomboa. Hata kata nyingi zilikuwa ngome ya upinzani, lakini tumezikomboa. Sasa kama zilizopotea hizo mbili, mimi nahusika vipi?”


Tuhuma kama hizo zilielekezwa kwa Profesa Juma Kapuya, ambaye licha ya kupitishwa na CCM kugombea ubunge wa Jimbo la Kaliua, anatuhumiwa kujinadi yeye na Magufuli, lakini akatumia usiku kumuombea kura Lowassa aliyegombea urais kwa tiketi ya Chadema.


Profesa Kapuya, ambaye aliangushwa kwenye jimbo hilo na Magdalena Sakaya wa CUF, alisema anaijua vyema CCM, hivyo asingeweza kufanya usaliti na kuendelea kubaki ndani ya chama hicho.


“Mungu pekee ndiye anayejua jinsi nilivyojituma kumuombea kura Dk Magufuli aliyekuwa mgombea wetu ambaye ameshinda na kuwa Rais. Sijui wanaonituhumu wanaanzia wapi,” alisema Profesa Kapuya.


Alisema hakukuwa na muda wa kufanya usaliti kwa sababu alikuwa anaachana na kamati ya kampeni usiku mara baada ya kumaliza vikao vya tathmini ya mikutano ya hadhara.


“Mtu kama mimi nitawezaje kufanya usaliti kama huo. (Nikifanya) Basi hapo shule itakuwa haijanisaidia,” alisema Profesa Kapuya ambaye amebobea kwenye elimu ya mimea.


“Pia ninaijua vyema CCM. Huwezi kuwa msaliti ukabaki kuwa salama huku ukiendelea kubaki hivyo. Ningejitoa mwenyewe.”


Tayari viongozi 21 wa Manyara wametimuliwa kwa tuhuma hizo.Kati ya waliotimuliwa, watatu ni kutoka Babati Mjini na wengine 18 wa ngazi ya kata.


Inadaiwa kuwa viongozi waliotimuliwa walikuwa wanamshabikia Lowassa na kusababisha CCM kupoteza jimbo na kata tano kati ya nane za Babati Mjini, kwa mujibu wa katibu wa CCM wa Manyara, Ndeng’aso Ndekubali.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post